Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah imesema imeonyesha sehemu ndogo tu ya uwezo wake wa kivita ambao umeushtua na kuudhalilisha utawala wa Kizayuni wa Israel.
Mwenyekiti wa ‘Mrengeo wa Muqawama’ (Mapambano ya Kiislamu)’ ambao ni tawi la kisiasa la Hizbullah katika Bunge la Lebanon amesema mafanikio ya ndege isiyo na rubani au drone ya Hizbullah, inayojulikana kama ‘Hassan’ ambayo ilijipenyeza katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel na kurejea Lebanon bila kutunguliwa ni mfano mdogo tu wa uwezo wa Hizbullah.
Muhammad Raad amepongeza oparesheni ya hivi karibuni ya drone hiyo ya Hizbullah na kusema ni moja kati ya mafanikio makubwa ya harakati hiyo na kuongeza kuwa hatua hiyo itaizuia Israel kutekeleza hujuma dhidi ya Lebanon. Amesema Hizbullah iko tayari kuilinda ardhi yote ya Lebanon pamoja na kuwa nchi hiyo inakumbwa na mgogoro wa kiuchumi.
Jeshi la utawala haramu wa Israel limekiri rasmi katika taarifa kwamba, licha ya silaha na zana zote za ugunduzi lilizonazo, likiwemo kuba la chuma, ndege za kivita na helikopta halikuweza kuigundua droni hiyo iliyotokea ardhi ya Lebanon siku ya Ijumaa.
Kufanikiwa ndege hiyo isiyo na rubani ya Hizbullah kuingia hadi ndani kabisa ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kumethibitisha kwa mara nyingine tena ufanisi duni wa mtambo wa ulinzi wa anga wa utawala haramu wa Israel unaojulikana kama Kuba la Chuma.