Mkuu wa Baraza Kuu la harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema ni makosa kwa baadhi ya nchi kutegemea uungwaji mkono na himaya ya Marekani, na kwamba kadhia ya Ukraine imethibitisha tena ukweli huo.
Akizungumzia vita vya Ukraine, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Hizbullah, Sayyid Hashem Safieddine amesema kuwa Lebanon itajiondoa katika majanga yote kwa ukombozi wa kweli na kujiondoa kwenye udhibiti wa utawala wa Marekani.
Ameongeza kuwa Marekani na nchi za Magharibi ziliwachochea Waukraini na kuwaahidi msaada na ushirikiano, lakini walipogundua kuwa maslahi yao yalikuwa hatarini, wamekengeuka ahadi zao na kulinda maslahi yao.
Mwenyekiti wa Baraza Kuu ya Hizbullah ya Lebanon ameeleza kuwa Rais wa Marekani, Joe Biden baada ya kuliona suala hilo kuwa zito ametangaza kuwa nchi yake haitashiriki katika vita vya Ukraine. Ameongeza kuwa: “Hivi ndivyo Marekani inavyowatumbukiza watu kwenye moto wa fitina nchini Lebanon kisha inawaacha mkono.”