Mazungumzo ya Russia na Ukraine mjini Belarus hayajulikani hatima yake

Televisheni ya taifa ya Russia imetangaza kuwa duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya wajumbe wa nchi hiyo na Ukraine imemalizika nchini Belarus, lakini haijafahamika iwapo mazungumzo hayo yataendelea au la.

Mazungumzo yana lengo la kuzima moto wa vita vilivyoanza Alkhamisi iliyopita kati ya nchi hizo mbili.

Awali mkuu wa timu ya mazungumzo ya Russia huko Belarus alitangaza utayarifu wa Moscow wa kufikia makubaliano na Ukraine haraka iwezekanavyo.

Sambamba na jitihada zinazofanywa ya timu za mazungumzo ya Russia na Ukraine chini ya upatanishi wa Belarus ili kukomesha mzozo huo, moto wa vita bado unaendelea kufukuta na ripoti zinaonyesha kuwa mji wa Berdiansk umetekwa na jeshi la Russia.

Wakati huo huo mashambulizi ya makombora yanayofanywa na jeshi la Ukraine na makundi ya kitaifa yenye msimamo mikali yanaendelea dhidi ya maeneo ya makazi ya raia huko Donbas, huku majeshi ya Russia yakichukua udhibiti wa mji wa kusini mashariki wa Berdyansk katika siku ya tano ya operesheni za kuilazimisha serikali ya Ukraine kusitisha mashambulizi dhidi ya wakazi wa Donbas.

Mkuu wa timu ya Russia katika mazungumzo hayo Vladimir Medinsky amesema leo Jumatatu kwamba “Ikiwa mzozo wa Ukraine utaendelea, idadi ya wahanga itaongezeka, kwa hivyo tunataka kufikia makubaliano haraka iwezekanavyo, na bila shaka makubaliano haya yanapaswa kuwa na maslahi ya pande zote mbili.”

Mapigano ya mitaani yanaendelea baina ya wanajeshi wa Ukraine na vikosi vya Russia katika mji mkuu Kyiv.

Mashambulizi ya jeshi Russia yalianza Alkhamisi iliyopita baada ya Rais Vladimir Putin wa Russia kutangaza kwamba jeshi la nchi hiyo limeanzisha “operesheni maalumu ya kijeshi” katika eneo la Donbass nchini Ukraine na kwamba lengo la operesheni hiyo ni kuiondoa Ukraine katika hali ya kijeshi na kwamba hana nia ya kuvamia ardhi ya nchi hiyo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *