Zelenskyy alisema hayo siku ya Ijumaa katika hotuba yake maalumu na kuongeza kuwa, hivi sasa mtu yeyote atakayeuawa nchini Ukraine, basi nchi za Magharibi zinabeba dhima ya kifo chake.
Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine amehamakishwa mno na uamuzi wa Jeshi la Nchi za Magharibi NATO kukataa ombi lake la kutangaza eneo lililo marufuku kupaa ndege na kuziambia nchi wanachama wa NATO kwamba, hivi nyinyi hata mna uwezo wa kulinda usalama wa nchi zenu?
Amesema, kitendo cha NATO cha kukataa ombi lake ni sawa na kutoa idhini kwa Russia ya kushambulia inavyotaka miji ya Ukraine.
Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg jana Ijumaa alisema kuwa, licha ya viongozi wa Ukraine kuomba kwa kusisitiza kwamba nchi za Magharibi zitangaze eneo lililo marufuku kupaa ndege huko Ukraine ili kupunguza nguvu za kijeshi za Russia, lakini NATO haitotangaza eneo kama hilo nchini Ukraine.
Zelenskyy amekasirishwa mno na matamshi hayo na amemwambia Katibu Mkuu wa NATO kwamba: Kuanzia leo wewe unabeba dhima ya kila mtu anayeuawa nchini Ukraine. Ameongeza kuwa, nashindwa kujua sasa nyinyi mnaweza kumlinda nani, hivi tukiangalia ule uhakika wa mambo, mnaweza kweli nyinyi hata kulinda usalama wa nchi zenu?
Rais wa Ukraine amezidi kufichua udhaifu wa Jeshi la Nchi za Magharibi NATO na kusema kuwa, kitu pekee mlichoweza kufanya hadi hivi sasa, ni kuipa Ukraine tani 50 tu za mafuta. Amesema, kama Ukraine itashindwa katika vita na Russia, basi madhara yake yatakuwa ni kwa nchi zote za Ulaya.