Kutekelezwa oparesheni ya kuvunja mzingiro dhidi ya Yemen ndani ya ardhi ya Saudia

Brigedia Jenerali Yahya Saree, Msemaji wa Jeshi la Yemen mapema wiki hii alitangaza kuhusu kutekelezwa oparesheni ya kuvunja mzingiro dhidi ya Yemen iliyotekelezwa ndani ya ardhi ya Saudia.

Kwa upande wa jiografia, oparesheni hiyo ya kuvunja mzingiro imetekelezwa huko Riyadh na pia katika maeneo ya kusini mwa Saudi Arabia yanayopakana na Yemen. Aidha kwa upande wa shabaha, oparesheni hiyo imetekelezwa dhidi ya taasisi ya Aramco huko Riyadh na pia Jizan na Abha; jambo linaloonyesha namna jeshi la Yemen linavyozishambulia taasisi nyeti za Saudi Arabia na hivyo kuuweka mashakani usalama wa kiuchumi wa Saudia.

Hapa kuna nukta kadhaa za kuzingatia na muhimu kuhusu oparesheni hiyo tajwa ya kuvunja mzingiro iliyotekelezwa huko Saudia. Mosi ni kuwa, oparesheni hiyo ni hatua halali kabisa; kama alivyosisitiza Brigedia Jenerali Yahya Saree Msemaji wa Jeshi la Yemen. Hatua hiyo inachukuliwa kuwa halali kwa sababu ni kitendo cha kujihami kutokana na kuwa utawala wa Saudia mwezi mmoja wa hivi karibuni umetekeleza mashambulizi mengi dhidi ya wananchi wa Yemen; ambapo wahanga wakuu wa mashambulizi hayo ni raia wa kawaida wa Yemen. Takwimu za Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF)  zinaonyesha kuwa watoto wa Kiyemen 47 wameuawa katika mashambulizi ya vikosi vamizi vya Saudi Arabia katika kipindi cha miezi miwili ya karibuni. Jeshi la Yemen na makundi ya kujitolea ya wananchi wa Yemen yaliitahadharisha Saudia mara kadhaa baada ya mashambulizi yake hayo dhidi ya raia wa Yemen hata hivyo iliendeleza mashambulizi na kupuuza tahadhari hizo za Yemen. Kwa msingi huo Wayemen wamechukua hatua za kuishambulia taasisi ya mafuta ya Saudia ya Aramco na maeneo mengine ya kimkakati ya nchi hiyo kama Riyadh, Jizan na Abha kama ilivyoitahaharisha Riyadh kabla.

Suala jingine ni kuwa, kama jina lenyewe la oparesheni linavyojieleza ni oparesheni ya kuvunja mzingiro. Wayemen tokea tarehe 26 Machi mwaka 2015 ambapo muungano vamizi chini ya uongozi wa Saudia na washirika wake  ulipoanzisha mashambulizi na vita dhidi ya nchi yao kila siku wanakabiliwa na hujuma za nchi hizo vamizi huku nchi hiyo ikiwa chini ya mzingiro wa pande zote wa Saudia. Hata hivyo hakuna hatua yoyote ilicyochukuliwa kimataifa kwa ajili ya kuvunja mzingiro huo tajwa dhidi ya Yemen licha ya uvamizi wa Saudia na washirika wake katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu. Kuwekwa mzingiro wa pande zote dhidi ya Yemen kumekuwa na madhara na maafa makubwa kwa nchi hiyo. Moja ya madhara hayo ni kuenea pakubwa magonjwa mbalimbali nchini humo; ambapo kimsingi hivi sasa ni vigumu na haiwezekani kuangiza katika nchi hiyo dawa kutoka nje. Aidha ni jambo lisilowezekana kutuma Yemen misaada ya kibinadamu kama bidhaa za chakula. Wananchi wa Yemen mbali na kuuliwa na kujeruhiwa katika mashambulizi ya kila uchao ya muungano vamizi wa Saudia; sehemu kubwa ambayo kwa mujibu wa takwimu ni mara tano ya vifo vilivyosababishwa moja kwa moja na vita, ni natija ya umaskini, njaa na magonjwa viliyowasibu wananchi ambao wamepoteza maisha katika kipindi cha miaka saba iliyopita ambayo ni natija ya mzingiro wa pande zote dhidi ya Yemen.

Ndio maana baada ya mashambulizi yaliyotekelezwa ndani ya ardhi ya Saudi Arabia miezi iliyopita ambayo lengo lake kuu lilikuwa ni kujihami hivi karibuni pia Wayemen wametekeleza oparesheni ya kuvunja mzingiro ambayo inahesabiwa kuwa ni lengo jipya. Huko nyuma Wayemen walikusudia kuzuia mashambulizi ya kila uchao ya Saudia dhidi yao kupitia oparesheni zao hizo hata hivyo hivi sasa kwa kutekeleza oparesheni hizo za kuvunja mzingiro wanataka kuuweka chini ya mashinikizo utawala wa Aal Saud ili uvunje mzingiro dhidi ya Yemen; hatua inayohesabiwa kuwa lengo lenye umuhimu mkubwa.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *