Mahakama ya India yaidhinisha rasmi uamuzi wa Marufuku ya hijabu katika skuli za serikali

Siku kadhaa baada ya skuli za jimbo la Karanatka la kusini mwa India kuwapiga marufuku wanafunzi wanawake Waislamu kuvaa vazi la staha la Kiislamu la Hijabu, mahakama ya nchi hiyo imeidhinisha rasmi uamuzi huo.

Tangu mwezi uliopita wa Februari, utekelezaji marufuku ya kuvaa hijabu katika skuli za jimbo la Karanatka lililoko kusini mwa India umekuwa ukilalamikiwa na kupingwa vikali na jamii ya Waislamu wa kila pembe ya nchi hiyo. Waislamu wapatao milioni 200 ni sehemu ya jamii kubwa ya India yenye jumla ya watu bilioni moja na milioni 400.

Vyombo vya habari vimeripoti kutoka Bangalore kuwa, baada ya siku kadhaa za uchunguzi na uhakiki, mahakama kuu ya jimbo la Karanatka leo imetangaza rasmi kuwa marufuku ya hijabu kwa wasichana Waislamu wanaosoma katika skuli za jimbo hilo ni sahihi kisheria.

Kupitishwa rasmi kisheria uamuzi huo kumefanyika ilhali jamii ya Waislamu walio wachache katika jimbo hilo imelalamikia vikali marufuku hiyo ya hijabu.

Tangu mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2021, uvaaji wa vazi la staha la Kiislamu la hijabu umezusha mvutano katika jimbo la Karanatka. Skuli kadhaa za jimbo hilo zilijichukulia uamuzi wa kupiga marufuku uvaaji wa vazi hilo kwa wanafunzi wa kike.

Uongozi wa skuli hizo uliwatangazia wanafunzi Waislamu kuwa, kama wanataka kuvaa hijabu hawatokuwa na haki ya kuingia madarasani. Wanafunzi hao walianzisha mikusanyiko na maandamano kulalamikia uamuzi huo, maandamano ambayo baadaye yalisambaa hadi kwenye miji mikubwa kadhaa ya India na hata ya nchini Pakistan.

Katika miaka ya karibuni, serikali ya waziri mkuu wa India Narendra Modi imewawekea mibinyo na vizuizi vikubwa Waislamu wa nchi hiyo. Sera ya serikali ya New Delhi ya kuwakandamiza Waislamu na kuwanyima haki zao imewashajiisha Wahindu wenye chuki kutumia fursa ya uungaji mkono ya chama tawala chenye misimamo mikali na ya utaifa cha BJP, kufanya vitendo vya mauaji na kumwaga damu za Waislamu wasio na hatia wa nchi hiyo…/

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *