Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ameilaumu NATO kwa vita vya Russia nchini Ukraine

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ameilaumu NATO kwa vita vya Ukraine na kusema kuwa atapinga wito wa kuilaani Russia. Matamshi haya ya Ramaphosa yanatia shaka iwapo atakubaliwa na Ukraine au nchi za Magharibi kama mpatanishi katika mzozo huo.

Ramaphosa ambaye alikuwa akizungumza bungeni, amesema: “Vita hivyo vingeweza kuepukika kama NATO ingezingatia maonyo kutoka kwa viongozi na maafisa wake kwa miaka mingi kwamba upanuzi wa shirika hilo la kijeshi kuelekea Mashariki ungesababisha hali ya kukosekana utulivu.

Hata hivyo amesisitiza kuwa Afrika Kusini “haiwezi kuunga mkono matumizi ya nguvu na ukiukaji wa sheria za kimataifa.”

Ramaphosa pia ameeleza kuwa Rais Vladimir Putin wa Russia amemhakikishia yeye binafsi kwamba mazungumzo yalikuwa yanaendelea baina ya nchi hiyo na Ukraine.

Kiongozi huyo wa Afrika Kusini amesema bado hajazungumza na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, lakini yuko tayari kufanya hivyo.

Ijumaa ya leo Ramaphosa amesema Afrika Kusini imeombwa kuwa mpatanishi katika mzozo wa Russia na Ukraine ingawa hakusema ni nani aliyemuomba aingilie kati.

Chama cha Ramaphosa cha African National Congress (ANC), ambacho kimetawala Afrika Kusini tangu utawala wa weupe walio wachache ulipokomeshwa nchini humo mwaka 1994, kilikuwa na uhusiano mkubwa na Muungano wa Kisovieti, ambao ulitoa mafunzo na kuunga mkono wanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi wakati wa Vita Baridi.

Rais Vladimir Putin wa Russia ametaja hatua za nchi hiyo huko Ukraine kuwa ni “operesheni maalumu” ya kupokonya silaha, kuiondoa Ukraine katika unazi mamboleo na kukabiliana na uchokozi wa NATO.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *