Spika wa Bunge la Uganda, Jacob Oulanyah aaga dunia

Spika wa Bunge la Kitaifa la Uganda, Jacob L’Okori Oulanyah amefariki dunia akitibiwa nchini Marekani.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda ametangaza kifo cha Oulanyah kupitia taarifa aliyoituma leo katika ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter inayosema kuwa: Wananchi wenzangu, nasikitika kutangaza kifo cha Mheshimiwa Jacob Oulanyah, Spika wa Bunge (la Uganda). Nilipokea habari hizi za kuhunukisha mwendo wa saa nne na nusu asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki kutoka kwa watu waliokuwa karibu naye na daktari aliyekuwa akimtibu.

Rais Museveni amesema amelazimika kuchelewa kutangaza kifo cha kada huyo maarufu wa chama tawala NRM, ili kusubiri watoto wake wajulishwe kwanza habari hizo.

Mara ya mwisho kuonekana Bungeni Spika Oulanyah ilikuwa Disemba mwaka jana 2021, ambapo aliongoza vikao vichache kikiwemo kile cha kupasisha kuwa sheria muswada wa Hazina ya Kitaifa ya Mafao (NSSF).

Alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Uganda mwezi Mei mwaka jana, na kumbwaga aliyekuwa bosi wake, Rebecca Kadaga, pamoja na Mbunge wa Manispaa ya Kira, Ibrahim Ssemujju.

Aliambuliwa kura 310, huku aliyekuwa Spika wa Bunge la Uganda, Rebecca Kadaga akipata kura 197, na Mbunge Ssemuju akipata kura 15 tu.

Alipopelekwa mjini Seattle katika jimbo la Washington nchini Marekani kwa ajili ya matibabu, raia wa Uganda wanaoshi nchini humo walifanya maandamano ya kulaani safari hiyo inayodaiwa kugharimu dola 500,000 za Marekani.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *