Mamia ya waandamanaji nchini Sudan wamefunga mitaa kadhaa katika mji mkuu, Khartoum leo Jumanne, wakishinikiza kuondoka madarakani utawala wa kijeshi na kuanzishwa utawala wa kiraia na kidemokrasia nchini humo.
Watu walioshuhudia wanasema, waandamanaji hao wamefunga mitaa mikubwa ya Khartoum, Bahri (Kaskazini) na Omdurman (Magharibi), kwa kutumia vizuizi vya zege, mashina ya miti na matairi yanayowaka moto.
Hatua hiyo imechukuliwa kwa wito wa “waratibu wa kamati za upinzani” katika mkondo wa kudai utawala kamili wa kiraia.
Hatua hii ya leo inafuatia maandamano makubwa yaliyofanyika jana katika miji kadhaa ya Sudan chini ya kauli mbiu “kurejesha hadhi ya walimu,” kuelekea Ikulu ya Rais.”
Jumuiya ya Madaktari wa Sudan imetangaza kuwa kijana mmoja aliyekuwa na umri wa miaka 17 aliuawa kwa kupigwa risasi na askari usalama katika maandamano ya jana kwenye mji wa Omdurman.
Jumuiya ya Madaktari wa Sudan imesema leo kwamba jumla ya watu waliojeruhiwa kwa kupigwa risasi katika maandamano ya jana, Jumatatu, katika miji ya Khartoum na Madani (katikati), walikuwa raia 173.
Idadi ya waliouawa katika maandamano ya kudai utawala wa kiraia nchini Sudan imefikia 89.
Kwa miezi kadhaa sasa, wananchi wa Sudan wamekuwa wakiandamana katika mji mkuu Khartoum na miji mingine mikubwa ya nchi hiyo kupinga utawala wa kijeshi wa nchi hiyo.
Waandamanaji hao wamekuwa wakishinikiza kurejeshwa serikali ya kiraia nchini Sudan sambamba na kupinga utawala wa kijeshi tokea Oktoba 25 mwaka jana.