UJUMBE wa Muungano wa Ulaya (EU) nchini Tanzania umeirai Afrika kuisaidia dhidi ya dhuluma na ukatili unaoendeshwa na Urusi nchini Ukraine.
Wito huo ulitolewa jana jijini Dar es Salaam na mabalozi wanane wanaoziwakilisha nchi za Poland, Ufaransa, Finland, Ujerumani, Italia, Uholanzi, Uswidi na Uhispania. Balozi wa EU nchini Tanzania, Manfredo Fanti, pia alikuwa kwenye kikao hicho.
Wito huo unajiri wakati baadhi ya nchi za Afrika zimekuwa zikikwepa kupiga kura kuhusu suala hilo lilipowasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) Machi 1.
Akiongoza ujumbe huo, balozi wa Ufaransa, Nabil Hajlaoui, alieleza sikitiko lake kuhusu hatua ya Urusi kuivamia Ukraine.Balozi huyo alisema Ufaransa inakashifu vikali ukiukaji wa demokrasia na haki za binadamu unaoendeshwa na Urusi.
Aliiomba Afrika kujiunga na Ulaya kukashifu ukatili huo, akisisitiza kuwa lazima taifa hilo liheshimu sheria za kimataifa.
Bw Fanti alisema kuwa Ulaya imeonyesha msimamo wa pamoja kuikashifu Urusi. Alisema anaamini kuwa kupitia juhudi za pamoja duniani, hali ya amani itarejeshwa Ukraine.
Balozi wa Poland, Krzysztof Buzalski, alionya kuhusu ongezeko la mgogoro wa kibinadamu nchini Ukraine, akisema kuwa ikiwa hali hiyo haitashughulikiwa, kuna hatari idadi ya wakimbizi kuongezeka hadi kufikia milioni nane.
“Kwa sasa, kuna zaidi ya watu 3.5 milioni walioachwa bila makao Ukraine huku baadhi yao wakitafuta hifadhi katika nchi jirani kama Poland,” akasema.
Mabalozi hao walisema ikiwa Afrika itajitokeza kuiunga mkono Ulaya kukashifu uvamizi huo, hilo litaonyesha ongezeko la ghadhabu ya dunia dhidi ya Urusi.
Kuhusu madai ya kubaguliwa kwa Waafrika wanaotoroka vita vya Ukraine, Bulzalski alisema Ulaya imeungana pamoja kukashifu vitendo vyovyote vya ubaguzi.
Alisema vitendo hivyo vinapaswa kukashifiwa vikali kwani ni sawa na kumdhalilisha mwanadamu.
Kuhusu hatua ya Tanzania na mataifa mengine ya Afrika kukwepa kupiga kura kukashifu uvamizi wa Urusi, walisema wanaheshimu uamuzi huo, japo wanaamini itakuwa bora ikiwa Afrika itaungana nao kuikashifu Urusi.
Hilo lilijiri huku Rais Joe Biden wa Amerika akiungana na viongozi wengine wa nchi za Magharibi kwenye mkutano wa siku tatu kujadili kuhusu suala hilo jijini Brussels, Ubelgiji.
Shirika la Kujihami (NATO), mataifa ya G7 na EU yanaandaa mikutano tofauti kuonyesha umoja wa nadra dhidi ya Urusi.
Rais Biden atahudhuria mikutano hiyo mitatu. Ni mara ya kwanza kwa rais wa Amerika kuhudhuria kikao cha EU jijini Brussels.
Wadadisi wanasema ziara ya Rais Biden haipaswi tu kuangaliwa kama hatua ya Amerika kuikashifu Urusi.
Wanasema uvamizi huo umeipa NATO na washirika wake mwamko mpya wa kijeshi.
Wanasema kuwa huku EU ikiendelea kukaka ushirikiano wake na Urusi, inahitaji kubuni ushirikiano mwingine, hasa baina yake na Amerika.
Inatarajiwa Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine atahudhuria vikao hivyo vyote kwa njia ya video.
Inatarajiwa marais na mawaziri mkuu 30 kutoka nchi zote za NATO wataunga mkono juhudi za kuisaidia Ukraine, zikiwemo kutumwa kwa majeshi zaidi.
Baadhi ya nchi hata hivyo zimeonyesha tashwishi kuhusu ombi la kutoa usaidizi wa silaha za kivita.
Licha ya kuahidi kuisaidia Ukraine, mataifa hayo yalisema hayaungi mkono ombi la taifa hilo kuungwa mkono kuweka marufuku ya ndege yoyote kupaa katika anga yake.