Kenya imezindua waya wa sita wa kusambaza intaneti upitiao baharini, hali ambayo imeletea wananchi matumaini kuwa huenda gharama ya kununua data ya simu ikapungua huku kasi ya intaneti ikiongezeka siku za hivi karibuni.
Kuzinduliwa kwa waya unaouanganisha Pakistan, ukanda wa Afrika Mashariki na bara Uropa (Peace) Jumanne, kunajiri wakati ambao uchumi wa intaneti nchini unakua kwa kasi.
Huku mahitaji ya kuhifadhi data kwenye mtandao, kutazama video moja kwa moja mitandaoni, masomo ya kidijitali na biashara mitandaoni na mifumo ya huduma za afya yakiongezeka, waya huo mpya unatarajiwa kuongeza thamani ya uchumi wa kidijitali.
Teknolojia hii yenye uwekezaji wa Sh46 bilioni inaunganisha Africa, Ufaransa na Pakistan kupitia njia ya bara uropa hadi Asia.
Waya huo utapunguza kuchelewa kwa mawasiliano kati ya bara la Afrika na Asia. Ni uzinduzi ambao ni ushirikiano kati ya Peace na Telkom, ambayo ni mtoaji wa huduma za intaneti kwa bei nafuu zaidi hapa nchini.
Waya huo wenye urefu wa kilomita 15,000 unatarajiwa kuongeza muunganisho wa kidijitali na kuletamtandao wenye kasi ya hadi gigabaiti 200 kwa kila sekunde.
Akizungumza katika uzinduzi huo eneo la Nyali, Mombasa, Waziri wa Teknolojia ya Mawasiliano ya Habari na Masuala ya Vijana, Bw Joe Mucheru alieleza kuwa Kenya ipo katikati mwa Mageuzi ya Nne ya Viwanda(4IR) ambapo mahitaji ya mtandao wa kasi upo juu kila wakati.
“Sasa hivi ukiwa kwenye Bustani ya Uhuru, unaweza kufurahia data yenye kasi ya 5G. Uzinduzi huu utabadili jinsi ambavyo Wakenya wanatumia mtandao. Idadi ya watu wenye simu za 5G pia inaongezeka, na waya huu tunaouzindua utahakikisha nafasi za biashara zinaongezeka maradufu,” alisema Bw Gicheru.
Afisa mkuu wa mipango ya Peace Cable Bw Sun Xiaohua alieleza kuwa ongezeko la hitaji la uunganishi na data litafungua soko mpya katika vituo vya kusambaza data, mitandao ya kutengeneza maudhui na kuwapiga jeki watoaji wakubwa wa intaneti nchini.
“Peace itahakikisha Wakenya wana chaguo kadhaa ifikapo kwenye uunganisho wa kidijitali. Itawapa mtandao wenye kasi sana, wenye uwezo na dhabiti ambao utapatikana katika sehemu nyingi nchini,” alisema.
Telkom ilieleza kuwa uwekezaji katika nyaya hizo zinazopitia chini ya maji ni muhimu sana kwa biashara zake kwani mtandao ni haki muhimu kwa kila mtu.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Telcom, Bw Mugo Kibati alisema kuwa ni muhimu kuchangia kwenye mikakati ya kugeuza Kenya kuwa ya uchumi wa kidijitali. Alieleza kuwa mitandao ikitumika ipaswavyo, itaboresha maisha ya Wakenya.
“Waya huu wenye uwezo wa hali ya juu utasaidia Kenya na eneo zima la Afrika Mashariki, kufikia malengo ya sasa na ya mbeleni ya kusambaza intaneti yenye kasi. Isitoshe itasaidia watoajihuduma kuwapa Wakenya mtandao bora kwa bei nafuu,” alisema Bw Kibati.
Bw Mugo aliongeza kuwa hatua hiyo ambayo inaboresha miunganisho ya data zinazoingia na kutoka Afrika mashariki, itarahisishaa shughuli ya kutua kwa nyaya nyingine za kusafirisha data ndani na nje ya eneo hilo.
Telkom kwa sasa inaendesha na kudumisha nyaya tano kati ya sita zipitazo chini ya Bahari Hindi ambazo zimetua nchini.
“Tunapanua uwezo wetu wa 4G katika eneo la Pwani, kabla ya kuhamia maeneo mengine ya huku nchini. Uwekezaji wa Sh14 bilioni kote nchini ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa upanuzi wa mtandao,” alisema Bw Kibati.
Katibu mkuu wa zamani wa ICT na mwenyekiti wa Jopokazi la Blokcheni na Teknolojia za Kiotomatiki Prof Bitange Ndemo ambaye ameshuhudia nyaya zote sita zikitua Mombasa alieleza kuwa Kenya iko tayari kukabana koo na mataifa magwiji wa teknolojia duniani.
“Ni haki ya kila mtu kufurahia intaneti. Kutua kwa waya wa sita ni ishara kuwa tuko katika njia sawa kiteknolojia. Nina uhakika tutashuhudia waya wa saba na hata wa nane ukitua,” alisema Prof Ndemo.