Hatimaye Kibaki Azikwa Karibu Na Kaburi La Mama Lucy

RAIS wa tatu wa Jamhuri ya Kenya, Stanley Emilio Mwai Kibaki alizikwa Jumamosi nyumbani kwake Othaya, Nyeri.

Mazishi ya Mzee Kibaki yalihudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta, naibu wake, William Ruto, kiongozi wa ODM, Raila Odinga ambaye alihudumu kama Waziri Mkuu katika serikali ya mseto iliyoongozwa na marehemu, makamu wake, Kalonzo Musyoka, miongoni mwa wanasiasa na viongozi wengine mashuhuri serikalini na pia kutoka nje ya nchi.

Alizikwa katika kijiji cha Thunguri, eneo la Othaya, kando ya kaburi la mke wake, Bi Lucy Kibaki aliyefariki Aprili 2016.

Aidha, katika kona za kaburi la Mama Lucy lina vyungu vinne vyenye maua.

Mila na desturi za jamii ya Agikuyu, anakotoka Mzee Kibaki, mwanandoa anapofariki endapo alikuwa ametanguliwa na mwenzake huzikwa karibu na karibu la mumewe au mkewe.

Ratiba ya mazishi iliongozwa na Askofu Mkuu Kanisa la Katoliki Jimbo la Nyeri, Anthony Muheria, na baada ya mapadre kumpa heshima za mwisho kwa kumwaga mchanga kaburini, familia ya karibu ya Mzee Kibaki ilifuata.

Rais Kenyatta na mkewe, Mama wa Taifa Bi Margaret Kenyatta, Naibu Rais Dkt Ruto na mkewe, Bi Rachael Ruto walifuata familia ya hayati, kisha Mkuu wa Majeshi, Robert Kibochi na maafisa wakuu katika idara ya jeshi – KDF.

“Mungu ailaze roho na nafsi yake mahali pema,” Askofu Muheria akabariki, baada ya kaburi kujazwa mchanga na kundi la vijana.

Baadaye, viongozi mashuhuri na wanafamilia wakaweka mashada ya maua juu ya kaburi hilo.

Mzee Kibaki aliongoza Kenya kati ya 2002 na 2013, ambapo amemiminiwa sifa tele kutokana na uongozi wake uliotajwa kuwa wa kishujaa katika kukomboa uchumi wa nchi na kutekeleza miradi ya maendeleo.

Kwa mujibu wa mila, desturi na itikadi za kikosi cha majeshi ya ulinzi wa Kenya, mizinga 19 ilifyatuliwa kama ishara ya heshima kwa Amiri Jeshi Mkuu huyo mstaafu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *