RAIS wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametangaza siku mbili za maombolezo nchini humo kufuatia kifo cha Rais wa Tatu wa Kenya Mwai Kibaki.
Maombolezo hayo ya kitaifa yanaanza leo Ijumaa Aprili 29 hadi Jumamosi 30, 2022.
Kwenye taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Rais Alhamisi, Aprili 28, Rais Suluhu aliwaomba Watanzania waungane na Kenya kuomboleza Hayati Kibaki ambaye atazikwa nyambani kwake Othaya, Nyeri, Jumamosi, Aprili 30, 2022.
Rais Suluhu pia aliamuru kuwa bendera zote za kitaifa nchini Tanzania zipeperushwa nusu mlingoti kwa heshima ya Kibaki aliyeongoza Kenya kuanzia mwaka wa 2002 hadi 2013.
“Katika kipindi cha siku mbili ya maombolezo ya kitaifa, bendera ya Tanzania itapeperushwa nusu mlingoti kote nchini na katika afisi za ubalozi wa Tanzania katika mataifa yote ya ng’ambo,” taarifa ya Ikulu ikasema.
Rais Suluhu alimtaja Kibaki kama kingozi mzalendo ambaye alichochea maendeleo ya kiuchumi nchini Kenya na hata Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
“Rais Samia anatuma rambirambi zake kwa wananchi wa Kenya na anatoa wito kwa Watanzania kuungana na majirani zao wakati huu mgumu wanapoomboleza aliyekuwa rais wao,” taarifa hiyo ikaongeza.
Suluhu ni rais wa pili wa taifa la Afrika Mashariki kutangaza siku ya kitaifa ya maombolezo kwa heshima ya Hayati Kibaki aliyefariki mnamo Ijumaa Aprili 22, 2022.
Mnamo Aprili 23, 2022, Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir ndiye alikuwa wa kwanza kutangaza siku tatu ya maombolezo kwa heshima ya Hayati Kibaki.
“Natuma rambirambi zangu kwa niaba ya serikali ya Sudan Kusini kwa Rais Uhuru Kenyatta na familia ya aliyekuwa Rais wa Kenya Hayati Mwai Kibaki. Kwa hivyo, natangaza siku tatu za maombolezo kote nchini Sudan Kusini,” ikasema taarifa kutoka Afisi ya Rais jijini Juba.
Rais Kiir pia aliamuru kwamba bendera ya Sudani Kusini ipeperushwe nusu mlingoti katika kipindi hicho chote cha maombolezo.