Wagombea ugavana na viti vingine vya kisiasa katika Kaunti ya Mombasa, wametia sahihi makubaliano mbele ya viongozi wa dini kwamba watadumisha amani katika kipindi chote cha uchaguzi wa Agosti.
Mkataba huo wa Amani, uliandaliwa na Baraza la Kitaifa la Makanisa ya humu nchini (NCCK), Baraza kuu la Waislamu nchini (SUPKEM), Kongamano la Mapadri wa Kikatoliki (KCCB) na Jukwaa la Makanisa jijini Mombasa (MCF).
Bw Hassan Omar anayewania ugavana kwa tiketi ya chama cha UDA, Awiti Bollo wa Vibrant Democtaric Party, mwaniaji mwenza wa tiketi ya ODM Francis Thoya kwa niaba ya Bw Abdulswamad Nassir na mgombea huru Daniel Munga Kitsao, ni miongoni mwa wawaniaji waliotia sahihi mkataba huo wa amani.
Mkataba huo uliwataka wawaniaji wa viti vya Ugavana, Useneta, Ubunge, Uwakilishi wa wanawake bungeni na MCA, kueneza amani wakati wa kampeni kwa maneno na vitendo.
Ulitaka pia waheshimu uhuru wa wapiga kura na wakubali matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.
Mkataba huo unafafanua kuwa endapo hawataridhika na matokeo ya uchaguzi kama yatakavyotolewa na Tume ya Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), watafute msaada mahakamani.
Kasisi wa Dayosisi ya Mombasa Martin Kivuva aliwaomba wawaniaji watumie manifesto na ajenda zao kutafuta kura na sio matamshi ya chuki wala vita.
“Wakati wa fujo umepitwa na wakati. Kwa sasa hatupigani kwa mapanga ila kwa sera za kuwatumikia wananchi,” alisema Kasisi Martin Kivuva wa Dayosisi ya Mombasa ambaye pia ni Mwenyekiti wa baraza la Wakatoliki.
Viongozi hao wa kidini waliwataka waumini wasiwaunge mkono, wawaniaji watakaoenda kinyume na makubaliano hayo ya amani.
“Si lazima umshushe mwenzako ndio wewe upande juu. Nataka kusema kuwa tumekubaliana na SUPKEM, KCCB, NCCK na MCF kuhusu mkataba huu. Kwa hivyo, yeyote atakayekwenda kinyume na mkataba huu, msimpe kura,” alisema Askofu Peter Mweru.
Mshirikishi wa SUPKEM eneo la Mombasa, Sheikh Khamis Mwaguzo aliwataka wawaniaji hao kuchukulia mkataba huo kwa uzito sana. Aliwataka viongozi wakumbuke kuwa uongozi unatoka kwa Mungu.
“Mkiwa hapa nyinyi kama wagombea, mumeonyesha heshima kwa viongozi wa dini na hata wakaazi wa Mombasa. Ila kumbukeni mnapopewa majukumu na wananchi kuwatumikia hakikisheni mnafanya kweli,” alidokeza Sheikh Mwaguzo.
Kando na kutia saini mkataba wa amani, wawaniaji viti mbalimbali walipewa nafasi ya kujipigia debe mbele ya waumini na wakaazi walioalikwa. Kulingana na viongozi hao wa kidini, wengi wao hawajulikani na raiya licha ya kuwania.
Shughuli hiyo iliyochukua takriban siku nzima, ilitumika kuwapa wakaazi nafasi ya kutangamana na wanaomezea mate viti mbalimbali vya uongozi na kufanya uamuzi.