Hizbullah ya Lebanon yaimarisha Jeshi lake katika kila upande, maandalizi ya kupambana na Wazayuni

Nguvu za Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon zimeongezeka kila upande, angani, ardhini na majini na imejiandaa kikamilifu kupambana na Wazayuni.

Hivi sasa harakati hiyo imejiweka tayari kukabiliana na utawala wa Kizayuni kikamilifu baada ya kuenea taarifa kuwa utawala huo pandikizi umekataa matakwa ya Lebanon ya kutoiba gesi katika eneo la nchi hiyo.

Shirika la habari la Ma’an la nchini Lebanon liliripoti habari hiyo jana Jumatatu na kuongeza kuwa, harakati ya Hizbullah imeongeza utayari wa timu zake za kutafuta taarifa za kiitelijensia na za kijeshi kuhusu shambulio lolote linaloweza kutokea. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Hizbullah imeongeza pia uchunguzi wake kuhusu namna ya kuangamiza vyombo vya majini vya Israel kama vita vitatokea.

Tovuti ya Lebanon 24 nayo imesema kuwa, matakwa muhimu na ya awali kabisa ya Hizbullah ni kuacha Israel shughuli zake zote katika maeneo ya gesi ya Lebanon na kadiri utawala wa Kizayuni unavyofanya ukaidi, ndivyo Hizbullah inavyozidi kujiweka tayari kwa ajili ya vita.

Kisima cha gesi cha Karish kiko katika mpaka nambari 29, baina ya Lebanon na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel. Beirut inaamini kuwa eneo hilo limo ndani ya ardhi ya Lebanon.

Hivi karibuni shirika moja linalodaiwa ni la Ugiriki limeanza operesheni za kutafuta gesi kwenye eneo hilo kwa kushirikiana na utawala wa Kizayuni wa israel hatua ambayo imetolewa onyo kali na Hizbullah ya Lebanon pamoja na viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *