Amir-Abdollahian: Iran inaamini kuwa kutatua matatizo ya eneo kutztokea ndani ya eneo lenyewe na sio nnje

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Iran inaamini kwenye kutatua matatizo ya eneo kutokea ndani ya eneo lenyewe na ameshukuru na kuthamini juhudi zinazofanywa na Iraq za kutilia nguvu mazungumzo na mchango wa nchi hiyo katika kuleta uwiyano wa kikanda na mazungumzo baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia.

Hadi sasa zimefanyika duru tano za mazungumzo kati ya Iran na Saudia katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, ambapo katika duru ya tano ya mazungumzo kati ya wawakilishi wa ngazi ya juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia umejitokeza mwanga mkubwa zaidi wa matumaini kuhusiana na kuanzishwa tena uhusiano baina ya nchi mbili.

Jana Jumapili, Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al-Kadhimi, akiandama na ujumbe wa ngazi ya juu wa nchi yake aliwasili mjini Tehran akitokea nchini Saudia na amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi ya juu nchini akiwemo Rais Ebrahim Raisi na Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian.

Katika mazungumzo na al-Kadhimi, Amir-Abdollahian ameeleza kuwa, kitu kipekee inachotaka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni heri kwa ajili ya eneo na inaunga mkono kufunguliwa tena balozi za Iran na Saudia katika miji mikuu ya nchi mbili.

Aidha, amegusia usitishaji vita nchini Yemen na kusisitiza uungaji mkono wa Tehran wa kuendelezwa usitishaji vita  na ulazima wa kuondolewa mzingiro wa kibinadamu iliowekewa nchi hiyo.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al-Kadhimi amegusia nafasi na mchango wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika matukio ya eneo na ukuruba uliopo baina yake na Iraq na akasema: Iraq ina nia ya adhati ya kustawisha uhusiano wa pande mbili na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Sambamba na kutilia mkazo kustawishwa uhusiano wa nchi mbili katika pande zote na udharura wa kuondolewa vizuizi vinavyoweza kujitokeza, al Kadhimi ameongezea kwa kusema: “tutaendeleza juhudi zetu kwa ajili ya kutilia nguvu mazungumzo na mashirikiano ya kikanda”

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *