Ripoti mpya ya shirika moja la kutetea haki za watoto imesema askari makatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewaua shahidi kwa kuwapiga risasi watoto 15 wa Palestina.
Shirika hilo la kimataifa la Defense for Children International tawi la Palestina (DCI-P) lenye makao yake mjini Geneva limesema, mbali na watoto 15 wa Kipalestina kuuawa na wanajeshi wa Israel tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, wengine sita wamejeruhiwa, huku wengine 17 wakitekwa nyara.
Aidha ripoti hiyo iliyotolewa na shirika hilo la DCI-P imesema watoto 16 wa Palestina wameachwa bila pahala pa kuishi, baada ya askari makatili wa Kizayuni kubomoa makazi yao, tangu Januari mwaka huu hadi sasa.
Shirika hilo la kutetea haki za watoto limesema utawala haramu wa Israel umeendeelea kufanya jinai hizo za kutisha za kuua, kujeruhi, na kukamata watoto wa Kipalestina mbele ya kimya cha jamii ya kimataifa.
Takwimu za shirika jingine la kutetea haki za watoto la +972 Magazine zinaonesha kuwa, mwaka jana 2021 ndio ulioshuhudia umwagaji mkubwa zaidi wa damu za watoto wa Palestina katika kipindi cha miaka 7 iliyopita.
Shirika hilo lilitangaza kuwa, watoto 86 Wapalestina waliuliwa shahidi mwaka jana na askari wa utawala wa Kizayuni katika eneo la Ukingo wa Magharibi, mji wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu pamoja na Ukanda wa Gaza.