Warioba: Katiba irudi kwa wananchi

ar es Salaam. Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesisitiza msimamo wake kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba akitaka maoni ya wananchi yapewe kipaumbele.

Warioba alisema hayo jana baada ya kutoa maoni yake katika Kikosi Kazi cha maoni ya demokrasia na vyama vya siasa, akitahadharisha maoni ya wananchi yasibezwe.

Pia alieleza akishangazwa kuona maoni ya viongozi na wasomi yakipewa msukumo mkubwa huku raia wa kawaida wakisahaulika.

“Katiba tumeanza mwanzo na tutafikia mwisho na mawazo yangu niliyatoa tunahitaji tu utashi wa kisiasa katika mchakato wote, sasa hivi naona mnachukua maoni ya viongozi na wasomi mnasahau maoni ya wananchi na mimi nafikiri imefika mahali viongozi wetu wakubaliane tupate Katiba inayotokana na maoni ya wananchi,” alisema Jaji Warioba.

Warioba aliyekuwa Mwenyekiti ya Tume Mabadiliko ya Katiba iliyokusanya maoni ya wananchi nchi nzima na kuunda rasimu mbili za Katiba, amekuwa akisisitiza kuhusu maoni hayo.

Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi Januari 6, 2022 jijini Dar es Salaam, alipendekeza kupatikana kwa Katiba mpya baada ya kushauri kupigwa kura za maoni mwaka 2024 wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Kuhusu mvutano wa ama uanze mchakato wa Katiba au kupatikana Tume Huru ya Uchaguzi, Jaji Warioba alisema hakuna sababu ya kuwepo kwa mvutano kwa sababu mchakato wa Katiba hauzuii sheria nyingine kupitishwa.

Jaji Warioba aliyekuwa mwenyekiti wa tume hiyo iliyoundwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete mwaka 2012, alisema mchakato huo ulikuwa karibu umefikia mwisho, baada ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi hadi Katiba inayoendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba.

“Baada ya kupitishwa (Katiba inayopendekezwa) ilikuwa iende kwenye kura ya maoni, lakini Jaji (Damian) Lubuva (aliyekuwa Mweyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi- NEC) akasema kwa sasa tunafanya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu,” alisema.

Huku akishauri viongozi wa vyama vya siasa wakutane kujadili jinsi ya kukamilisha mchakato huo, Jaji Warioba alisema, “mimi nimetoa maoni yangu, kwamba nafikiri ingefanywa mwaka 2024 kwa sababu ni mwaka wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ili kupunguza gharama. Tuchanganye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kura za maoni.”

Akemea ukabila

Katika hatua nyingine, Jaji Warioba alitahadharisha kuhusu mikutano ya machifu, ukabila, udini na ukanda, huku akitaka Watanzania kukemea vitendo hivyo kwani vikiachwa vinaweza kuligawa Taifa.

“Siku hizi nasikia kuna mikutano ya machifu sijajua wanaitoa wapi. Yarabi toba, sijajua akina Mangi Mkuu watarudi tena na watemi wale na babu yangu ni mkuu wa kabila langu, lakini akinialika kwenye mikutano hiyo sivutiwi nayo,” alisema.

Allisema alisema hali hiyo imekuwa kama fasheni inajitokeza zaidi linapojitokeza tukio vijana kwenye mitandao wamekuwa wakijadili kwa mitazamo ya ukabila.

“Naona katika nchi yetu tumeanza kuona viashiria ambavyo vinaweza vikavunja amani yetu, waasisi walijenga Taifa hili kwa umoja, tukawa na amani kwa kuondoa mambo yaliyokuwa yanatutenganisha.

“Ukabila, udini, ubaguzi wa rangi, ukanda kwa sasa naona yanarudi, na yamekuja mengine mapya tofauti za kisiasa, kwa hiyo tunakuwa na wananchi wakati mwingine hatuaminiani kwa sababu tuko katika makundi mbalimbali, hivyo nasema tujue sisi Watanzania nguvu tuliyonayo kuliko kitu kingine chochote ni umoja wetu na amani yetu,” alisema.

Kiongozi huyo alisema hata matatizo yanayozungumzwa sasa ikiwemo katiba ni kwa sababu Taifa limekuwa na umoja na amani ambayo misingi yake ilishajengwa na waasisi wa Taifa.

“Ukiona vijana kwenye mitandao likijitokeza tukio wanazungumzia katika mtazamo ama wa ukanda, udini au ukabila. Makabila yapo yamekuwapo wakati wote si kusema kwamba yaliondolewa, lakini tuliyokubaliana tuyaache na kama yanajitokeza tuchukue hatua kuyazuia yasiendelee ama tuyakemee.

“Lakini naona sasa inakuwa kama ‘fashion’ kuzungumzia kwa misingi ya ukabila, ukanda, vyama. Sisi Watanzania tunataka haya mambo yasitutenge, ukabila usitutenge, udini usitutenge ama ukanda usitutenge, tuwe Watanzania na umoja wetu na ndiyo msingi wa amani.

“Haya yanayotokea sasa ni dalili ya ukanda na ukabila umeingia sana mpaka tunafikia mahali tunaanza kuingiza mambo ya machifu, sasa tusije tukarudi kwenye misingi hiyo ya ukabila itakuja kutugawanya,” alisema Jaji Warioba.

Mangula

Naye Makamu Mwenyekiti wa CCM Mstaafu, Philip Mangula, alihimiza maridhiano yaendelee kufanyika, kwani hakuna linaloshindikana kwenye meza ya mazungumzo.

“Katika uzoefu wangu nimefanya maridhiano mara mbili yanayotokana na mgogoro na ikitokea hali hiyo lazima itafutiwe majibu kwa njia ya mazungumzo.

“Tumefanya maridhiano mwaka 2001 ulipotokea mgogoro kati ya CUF dhidi ya CCM, tulichukua muda hadi kuja kuelewana na mwanzo unakuwa mgumu siku zote, lakini kujenga hoja ni ufumbuzi wa tatizo,” alisema Mangula.

Kuhusu katiba mpya, mangula alisema ni vema wananchi wenyewe wakasikilizwa na kama kutakuwa na ulazima kujibu malalamiko wanayotoa.

“Mchakato wake ulishaanza na unakuwa na malengo ya kujibu changamoto fulani, mathalani katiba ya kwanza ilikuwa ya Uhuru 1961 baadaye tulikuwa na katiba ya muda mwaka 1965, kabla ya kuja na katiba ya chama kimoja na mwaka 1992. Tulibadilisha katiba kwa sababu ya vyama vingi vya siasa, hata sasa tunaweza kuangalia kama kuna uhitaji huo,” alisema Mangula.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *