Jaji Lubuva: Uteuzi wa vigogo Tume ya Uchaguzi utazamwe upya

Dar es Salaam. Mwenyekiti mstaafu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva ameishauri Serikali kuutazama upya utaratibu wa kupatikana kwa watendaji wakuu wa taasisi hiyo ili kutoa fursa kwa Watazania kuongeza imani na watumishi hao.

Katika mabadiliko hayo, jaji huyo mstaafu wa Mahakama ya Rufani, alisema ili kurejesha imani kwa chombo hicho kinachosimamia uchaguzi, kiundwe chombo kidogo, ambacho kitakuwa kinaongozwa na Jaji Mkuu na wajumbe wengine, ambao watakuwa wanawafanyia usaili watumishi wanaoomba kuongoza NEC.

Chombo hicho, amesema kinawashindanisha walioomba kwa vigezo na sifa zinazotakiwa kabla ya kuwasilisha majina ya watakaopenya kwa Rais kwa ajili ya uteuzi.

Akizungumza jana na wanahabari baada ya kutoa maoni yake kwenye kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, Jaji Lubuva alisema kwa hali ilivyo sasa, Watanzania wamekuwa na malalamiko na manung’uniko mengi juu ya utendaji kazi wa watumishi hao wa Tume ya Uchaguzi.

“Kuna malalamiko na minong’ono, watu wangependa makamishna wa Tume ya Uchaguzi utaratibu wake ubadilike, jambo ambalo hata mimi nalikubali, kwamba katika uchaguzi ni muhimu sana kuwe na imani na wahusika.

“Kwa hiyo katika hali hiyo nakubali uwezekano wa kuangalia utaratibu wa kuteuliwa kwa mwenyekiti na makamishna wa uchaguzi ili iwe tofauti na ilivyo sasa,” alisema Jaji Lubuva, aliyeongoza NEC kati ya mwaka 2011 na 2017.

“Wakisharidhika (kwamba) huyu au yule anatufaa kuwa mwenyekiti au kamishna, majina hayo ndiyo yapelekwe kwa Rais afanye uteuzi, hii itasaidia kuendana na imani ya wahusika,” alisema.

Hata hivyo, Jaji Lubuva ambaye amewahi kuwa mwanasheria mkuu wa Serikali wa muungano na Zanzibar kwa nyakati tofauti, alisema Tume ya uchaguzi imekuwa huru, japo imekuwa ikilalamikiwa kwamba si huru.

Alitolea mfano kipindi cha miaka mitano aliyodumu kwenye taasisi hiyo, kwamba hakuna hata siku moja tume hiyo iliwahi kuelekezwa na kiongozi yeyote katika kutekeleza majukumu yake.

“Tume ipo huru, mfano mwenyewe ndani ya kipindi cha miaka mitano nilichodumu kwenye taasisi hiyo haijawahi kuelekezwa na kiongozi hata mmoja, iwe Rais au Waziri Mkuu (kwamba) fanyeni hili au lie katika shughuli za tume,” alisema mwanasheria huyo aliyewahi pia kuongoza kamati ya uchaguzi ya nchi za SADC

“Nikiwa ndani ya kikosi kazi nimesisitiza hata uzoefu wangu kwa nchi za ukanda wa nchi za kusini mwa Afrika SADC, nilikuwa kule, nilikuwa mwenyekiti wa kamati ile, kwa kuona shughuli tuliyokuwa tunaifanya walikubali ingawa hatukujiita tume huru lakini kikazi na shughuli tulikuwa huru,” alisema Jaji huyo aliyewahi pia kuwa waziri wa Katiba na sherria.

Kuhusu Katiba mpya, kiongozi huyo mstaafu alishauri mchakato ulioanza na Jaji Joseph Warioba umaliziwe, huku akieleza mambo yaliyopitwa na wakati yabadilishwe ili wananchi wapigie kura Katiba.

“Katika kipindi ambacho nilikuwa msimamizi wa uchaguzi, Serikali ilileta rasimu ya katiba iliyokuwa imepitishwa na Bunge Maalumu kwenye Tume ya Uchaguzi ili tuweze kufanya kura ya maoni pamoja na uchaguzi mkuu, lakini kutokana na mambo yalivyokuwa, tusingeweza kusimamia uchaguzi wa kawaida na hii ya kura ya maoni, kwa hiyo tukaiachia pale na tulimweleza Rais.

“Katiba mpya tunavyoizungumzia sasa, isiwe kama tunaanza upya, tuendelee kutoka pale tulipoachia ile rasimu ya katiba iliyoachwa njiani, twende nayo ili iweze kupigiwa kura ya maoni, lakini kuna baadhi ya mambo yamepitwa na wakati, yale yanaweza kurekebishwa kwa kutumia sheria mbalimbali ili tuweze kwenda na mfumo huo wa kukamilisha Katiba mpya, lakini si kuanza upya.

“Watu wengine wanazungumza utadhani tunaanza upya, pale ambapo Bunge Maalumu limefanya kazi yake, Tume ya Warioba imepita nchi nzima kuchukua maoni, sasa kama kuna machache yamepitwa na wakati yanaweza kurekebishwa kwa kutumia sheria nyingine tuweze kuendelea kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya,” alisema.

Wasomi, wadau wafunguka

Wakizungumza na Mwananchi jana, baadhi ya wasomi na wadau wa siasa waliungana na wazo la Jaji Lubuva.

Mjumbe wa bodi ya Jukwaa la Katiba, Hebron Mwakagenda alisema ni kweli ili Tume ya uchaguzi iwe huru, wanaoiongoza wanapaswa kuomba na kufanyiwa usaili na kwa kufanya hivyo kutasababisha washiriki kwenye chaguzi wakiwa na imani na kuondo manung’uniko.

“Pamoja na yeye kudai hakupewa maelekezo yoyote wakati akiwa kwenye nafasi hiyo, anaona hatari inayoweza kujitokeza huko mbele, chombo cha usimamizi kutokuwa huru ni hatari kinaweza kusababisha machafuko,” alisema.

Kwa upande wa mwanasheria wa kujitegemea Pasience Mlowe, alisema kwa nchi zilizopiga hatua zina tume huru ya uchaguzi, lakini kwa Tanzania kuna tume ya taifa uchaguzi.

“Kutokuwa na Tume huru lolote linaweza kutokea, tumeona watu wenye sifa wakienguliwa bila sababu ya msingi, tumeona chaguzi zikifutwa bila kujua kama ni maelekezo au ni utashi wa mtu mwenyewe,” alisema Wakili Mlowe.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara) Benson Kigaila alisema msimamo wa chama hicho ni kupata Katiba mpya, kwani kinachoweza kuleta tume huru ni Katiba.

Alisema Tume iwe iwavyo, uhuru unapatikana na katiba pekee, na wala si kwa mawazo ya mtu kwani hata Katiba iliyopo inaeleza uchaguzi kutokupingwa mahakamani.

“Watu wanafikiri tunataka katiba kwa ajili ya uchaguzi ujao, hatutaki katiba kwa ajili ya Tume huru, tunataka Katiba ili kupigania haki za watu,” alisema Kigaila.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema ni sahihi watu hao (viongozi wa NEC) kuomba nafasi, na mwenye sifa ateuliwe, kutamfanya afanye kazi kwa uhuru.

Alibainisha Tume iliyopo hata ikitenda haki hakuna atakayeridhika, atakayepewa hiyo nafasi ni lazima kupendezesha mamlaka yake ya uteuzi.

Lakini Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie alisema mapendekezo aliyoyatoa ni katika hali ya kuleta imani kwenye chombo cha uchaguzi, hata watu wanaoshindandana mmojawapo asiposhinda, kutakuwa na imani na hakutakuwa na malalamiko na kufanya chombo hicho kufanya kazi bila hofu,” alisema.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *