Hotuba ya Ijumaa – 1 Julai 2022
Hujjatul Islam Ustad Syed Jawad Naqvi
(Mkuu wa shule Jamia Orwatul Wuthqa – Lahore)
Imetolewa: Msikiti wa Baitul Ateeq
Lahore – Pakistan
Hotuba ya 1: Tathmini ya Dini kwa mtizamo wa Imam Sajjad (a) – Sehemu ya 1
Ninawausieni nyinyi pamoja na kuiusia nafsi yangu kumcha Mwenyezi Mungu na nawasisitizieni kuyasimamisha maisha yenu katika misingi ya Uchaji Mungu (Taqwa). Ucha Mungu ni mipango na mikakati kutoka kwa Mwenyezi Mungu yenye kumlinda mwanadamu, mikakati anayopaswa kutekeleza katika maisha yake.
Ni sifa kamilifu inayohifadhi utu. Ikiwa Taqwa itakosekana katika nyanja muhimu za maisha ya mwanadamu, basi mwanadamu huyu atakumbana na majanga makubwa katika mambo yake ya kidini, kitaifa, na hata kijamii.
Hatari kubwa inayoikabili jamii ni tamaa ya uongozi. Hatari ambayo imezingira umma wote wa Kiislamu na haswa nchi ya Pakistan. Ambapo upendo wa madaraka, mamlaka na uongozi umeshamili watu wote.
Maimamu wamesema kuwa kupenda uongozi kunaharibu dini na utu wa wale wanaojiingiza humo.
Imamu Sadiq (a.s) anasema jihadhari, jiepushe na usuhuba na wale walionahamu ya uongozi. Je tunayachukulia kwa uzito mafundisho ya Maimamu au hatuyapi umuhimu wala hatuyaamini japo tunayasikiliza ilimradi tu tujizolee thawabu na zaidi ya hapo hatuyafanyi mafundisho haya kuwa ndio sera ya maisha yetu.
Kuna hatari ambayo Imam anaashiria anaposema “Wallahi, yeyote anayetaka kusikiliza sauti ya nyayo nyuma yake”. Wale wanaotaka kuwa viongozi na wakuu kama hivyo ili watu watembee nyuma yao na kuwapigia makofi. Watu hawa hawana uwezo wa kuongoza lakini wana tamaa ya uongozi.
Hakuna hata mmoja wa watawala wa zamani na wale wa hivi sasa nchini Pakistani aliye na uwezo wa uongozi na utawala bali wana tamaa, na mapenzi yao kwa uongozi yamepita mipaka.
Imamu anatueleza ni hatari gani inapayopatikana kutoka kwa mtu kama huyu akisema: “Mwisho wake wa uhakika ni kuangamia kwake yeye mwenyewe na wale wanaomfuata”. Uharibifu huu ni hatari na wakuu hawa ni viongozi wa upotovu na uharibifu, na uharibifu huu ni wa aina tofautitofauti.
Mtu anapokuwa kiongozi atambue kwamba Amirul Momineen (a.s) anasema kwamba balaa kubwa la kupenda uongozi ni kiburi. Hii ina maana ya kujivunia na kujionyesha kwa watu binafsi. Katika lugha ya kiarabu neno “Fakhr” maana yake ni chombo tupu kinachotoa kelele. Jamii ya Wapakistani ina watawala na viongozi watupu ambao hawana uwezo wowote wa kutawala isipokuwa utupu kutoka ndani. Watajiangamiza wenyewe pamoja na kuiangamiza jamii.
Kuna hadithi moja yenye maana pana sana kutoka kwa Imam Sajjad (a.s) ambayo inapaswa kuwa sera ya maisha yetu. Hadithi hii imo katika Kitabu Al-Ihtijaj Juzuu ya 2 ambapo imepokewa na Imam Ridha (a) japo Hadithi yenyewe inatoka kwa Imam Sajjad (a.s). Katika hadithi hii Imam (a) ameifafanua hadithi hii ili kuwatoa watu kutoka katika upotofu katika zama zile. Aya za Quran pia zinapaswa kuzingatiwa katika muktadha wa zama. Kila enzi ina mahitaji yake maalum.
Katika uteremsho wa Quran madai ya zama hizo na zama zijazo yote yalizingatiwa. Ni jukumu la mwanachuoni kuelewa aya ya Quran kwa kuzingatia zama zote mbili jambo ambalo mara nyingi hupuuzwa. Vile vile Hadithi zilizotoka kwa Mtume pia zinabeba mafunzo ya zama hizo, mahali husika na mafunzo ya wakati ujao. Mwanachuoni atafasiri kwa kuzingatia zama zote mbili, aangalie sifa makhsusi ya zama hizo na aone iwapo sifa hizo zinapatikana katika zama hizi au la. Kwa mfano Mtume amemwagiza mtu kuvaa blanketi au kutumia Meswak (mswaki).
Katika zama hizo dawa za meno na mswaki wakileo hazikuwepo. Utapata maana ya hadithi hii ni lengo la kupiga mswaki au kuvaa kitu wakati wa baridi. Sio kwamba tutafute vitu vile vile vya enzi hizo, ambavyo havipatikani katika zama hizi. Tunahitaji kupanua akili zetu na sio kuwa na fikra finyu. Mwongozo wa Maasumu hubeba thamani halisi japo tunatelekeza na kufuata nukuu za watu wengine.
Imamu Zainul Abideen (a) anasema (kutoka Al Ihtijaj – Juzuu ya 2, Hadithi nambari 152). Katika lugha ya Kiarabu neno “Ihtijaj” maana yake ni kukamilisha hoja na kuthibitisha jambo. Imamu anasema (a): “Ukimuona mtu ambaye mandhari yake ya nje ni yenye kuvutia; mfano sura yake, anadhihirisha utu, anaonekana kung’aa sana na kuna mvuto mwingi katika mazungumzo yake na tabia yake ma utamkuta ni mnyenyekevu na mwenye heshima sana.
Mtu kama huyo yapaswa kujihadhari naye usije ukahadaika. Kisha unapaswa kufanya nini? Imam (a) anasema tujizatiti kuweka sifa ya kumpima mtu.
Pamoja na hayo Hatuna budi kukumbuka kwamba hadithi hii inazungumzia zama za Imam Sajjad (a) ambazo zilikuwa zama nyeti sana. Wakati Imamu (a) anawaonya watu wasije wakahadaika na mandhari ya nje basi kulikuwa na watu kama hao ambao waliwahadaa watu na watu wengi kwa kutokujua walikuwa wakiwafuata. Kwa mfano wakati Imamu (a) yupo bado watu walimtelekeza na kumtenga huku wakimfuata Muhammad ibn Hanafiya na majina mengine makubwa kama Mukhtar a Thaqafi na kadhalika.
Ndiposa Imamu (a) anasema jihadhari na mtu ambaye mandhari yake ya nje yanaonekana ni mazuri, basi mandhari haya yasikudanganye.
Kuna wengi ambao ni wapenzi wa dunia lakini hawana namna. Hii ina maana hawafikii anasa za dunia sio kwa kuwa hawataki bali kwa vile hawana njia. Wanaonekana kuwa wingi wa zuhudi kwa sababu hawana uwezo wa kufanya dhambi.
Zuhudi sio kule kipofu kudai hajamuona Na-Mahram. Wale wanaofanya zuhudi ambao hawana ujasiri ni wenye pupa ya dunia na wanatamani kufanya Haramu wasiweze kwa udhaifu wao na si kwa sababu ya kujizuia, hawana nia thabiti ya kutofanya madhambi bali wanaogopa matokeo yake katika dunia hii.
Mtu dhaifu namna hii ambaye hatendi dhambi kutokana na kutokuwa na uwezo na ameufanya muonekano wake wa nje kuwa mzuri na ameifanya dini kuwa mtego wa panya. Ameitumia dini kuwatega waumini. Anaendelea kuwahadaa watu.
Imamu (a) anatutanabahisha akisema kwamba kuna watu kama hao ambao wako tayari kufanya jinai aina yoyote ili kuwahadaa watu kupitia dini.
Tunahitaji kuwatathmini kwa umakini watu wa karibu yetu ambao wanajiepusha na dhambi. Kuna watu wengi kati yao ambao wanangojea tu fursa ya kufanya uhalifu na pindi inapojitokeza fursa hufanya uhalifu haraka sana. Ninazungumzia sifa hii kwa sababu tunaingizwa kwenye msiba huo hii leo.
Imamu ametutanabahisha kuwa iwapo watu kama hao watajitokeza basi kwanza tunahitaji kuwapima na kisha baadae tuwaamini. Ni masikitiko kuwa tumepuuza usia huo halafu baada ya miaka minne hadi mitano tunasema wametudanganya. Imam hawaongoi wale wanaodanganya bali anawaongoza wale wanaodanganywa ili wasiteswe na wadanganyifu.
Basi ukimuona mtu anastahi katika mali ya haramu. Hii ina maana kuwa yeye ni mwangalifu sana juu ya mali ya Haram, basi jihadhari na usihadaike naye, asikudanganye. Hii ni kwa sababu tamaa ni ya aina tofautitofauti. Mtu Mwenye kujiepusha na mali ya haramu au kutokuwa na matamanio ya mali haimaanishi kuwa hana matamanio mengine.
Wapo wengi wanaopita kiasi kikubwa na kukataa, lakini mtu huyohuyo anayeepuka mali ya Haramu huenda akawa ameghubikwa na matamanio ya zinaa. Kisha ukimuona mtu ambaye katu hamuangalii asiyekuwa maharimu wake, jihadhari na yeye pia. Isipokuwa pindi unapoona ni mtu aliyesalimika kiakili, hii ni kwa sababu baadhi ya waliojiweka mbali na mali ya haramu au wanawake wasiokuwa maharimu wao wamefanya hivyo kwa sababu wao ni madhaifu kiakili na akili zao hazizingatii mambo haya. Ni wapumbavu, na haiwashiki mitego yao. Halafu hata ukimkuta ana akili na sio mjinga.
Hii ina maana mandhari yake ya nje ni mazuri, anajiepusha na mali ya Haram, Na wasiokuwa Mahram wake na si mjinga; basi pia jihadhari usije ukanaswa naye. Sasa sehemu ya mwisho inahitaji ufafanuzi baadaye ambapo Imam anasema Tathmini kama akili ndio yenye kutawala matamanio au matamanio ndio yanayoitawala akili.
Mwenyezi Mungu atujaalie uoni huo ambao Imamu Sajjad (a) anatuletea ili tubakie kulindwa kutokana na majanga ya zama zetu.
Hotuba ya 2: Kuitelekeza dini kwa ajili ya dunia hupelekea kwenye uharibifu
Hekima nambari 106
. وَ قَالَ عليه السلام: لَا يَتْرُكُ النَّاسُ شَيْئاً مِنْ أَمْرِ دِينِهِمْ لِاسْتِصْلَاحِ دُنْيَاهُمْ إِلَّا فَتَحَ اللَّهُ عَلَيْهِمْ مَا هُوَ أَضَرُّ مِنْهُ .
” Watu hawataacha jambo lolote lile linayohusiana na dini yao ili kurekebisha mambo yao ya kidunia, ila Mwenyezi Mungu huwafungulia jambo lilikowa na madhara zaidi kuliko hayo.
Tunapaswa kutumia maneno haya katika mazungumzo yetu ya kawaida. Kwa kawaida tunatoa nukuu za watu wengine basi kwa nini hatuwezi kutumia kauli hizi za Maasumin!
Riwaya inasema kwamba ili kuuweka sawa ulimwengu wao baadhi ya watu hunyanyua mikono yao na kutelekeza baadhi ya mambo muhimu ya kidini, kwao wao Mwenyezi Mungu huwafungulia mlango wa namna hiyo ambapo wanaangukia katika madhara na hasara nyingi zaidi kuliko madhara ya kujiepusha na dini.
Ili kuokoa ulimwengu wao, baadhi ya watu hupuuza mambo yao ya kidini kwa hisia kuwa wakifuata maamrisho ya kidini basi kazi zao na nyadhifa zao kubwa zitaathirika. Mambo haya yanaonekana wazi wazi kwa maafisa wakuu katika mashirika ya serikali. Hawaswali ili upandishaji wa vyeo kwao usitishwe.
Akionekana kuwa ni Shia, basi anakuwa muangalifu zaidi. Huko India msomi mmoja alikuwa akisema kwamba Waislamu wameficha utambulisho wao ili wapate kujilinda kutokana na msimamo mkali wa Wahindu. Kwa kuwa tu wako kwenye nyadhifa kubwa wameficha utambulisho kwa kunyoa ndevu zao, kutumia majina mafupi ya mbadala. Hayo yote kwa ajili ya kuokoa ulimwengu wao basi wameitelekeza dini. Imam Ali (a) anasema kwamba mtu anapochukua tabia hiyo Mwenyezi Mungu humuingiza katika madhara ambayo yanaangamiza ulimwengu wao.
Tunahitaji kuangalia kote kwa makini na kuona popote ambapo wote wameiasi dini kwa ajili ya kuokoa dunia yao, wameishia kujipata katika sintofahamu katika mahusiano yao ya kijamii.
Katika baadhi ya sehemu unapohifadhi utambulisho wako wa kidini huwezi kupata hata mapendekezo ya ndoa kutoka kwa familia nzuri ya kitajiri. Na ikiwa unataka kuondoka nchini kwenda nchi za kigeni unahitaji kuficha utambulisho wako wa kidini ili upate kazi. Vile vile katika maisha yako ya kiuchumi, kijamii, kisiasa inakubidi kuficha utambulisho wako wa kidini. Sio kwamba wanaficha, Amirul Muminin (a) anasema kwamba wanaasi utambulisho wao wa kidini na sio kujificha tu ili waweze kurekebisha mambo yao ya kidunia na ilhali ukweli ni kuwa ulimwengu wa watu hao hao unaangamizwa. siku hiyohiyo wanapoficha utambulisho wao basi ndio siku ambayo wanaiacha dini yao.
Mwenyezi Mungu ana utaratibu wake ambao kwao anawaangusha na kuangamia kwao kunafanyika kwa mujibu wa mfumo huo. Huo ni “Muhula” ambao ni miongoni mwa Sunna za Mwenyezi Mungu ambayo yeye ameiweka kwa ajili ya mwanadamu ambayo kwayo mwanadamu hupata uongofu au kuangamizwa. Utapata katika Quran pia baadhi ya watu wanauliza ni kwa nini madhalimu hawaadhibiwi na kuangamizwa!
Mfano huko Pakistani ambapo wananchi wana ghadhabu kubwa juu ya watawala wao, je ni kwa nini hawaangamizwi!
Sababu moja kuu ni kwa sababu baadhi ya wafuasi wao huipenda hali ile, hivyo basi watabaki kuwatawala. Chanzo kikuu cha mgawanyiko wa Umma wetu ni shetani na watu wasipo jitenga na watawala hawa madhalimu basi Mwenyezi Mungu atawaangamiza.
Mwenyezi Mungu anasema kwanza watu wabadili hali zao wenyewe ndipo Mwenyezi Mungu abadilishe hali zao.
Sheria ya pili ni kwamba Mwenyezi Mungu huwapa muhula madhalimu. Sheria ya tatu ni Istedraj (taratibu) ambapo Mwenyezi Mungu atawakamata hatua kwa hatua.
Kwa mfano baadhi ya maradhi humshambulia mwanadamu mara moja na dalili zake huonekana mapema lakini yapo yale yenye uharibifu mkubwa na hushambulia polepole na hatimaye kumwangamiza mwanadamu.
Hakika wale wanaoiacha dini, na kutekeleza majukumu yake, hawafanyi mazingira ya nyumba zao kuwa ya kidini na hawalei watoto wao kwenye misingi ya kidini bila shaka mwisho wao ni kwenye bonde la madhara na uharibifu lakini mambo hayo hufanyika taratibu.
Katika jamii zilizopita pia tunaweza kuona kwamba familia zilizokuwa na maisha mazuri ambazo ziliaasi dini kwa ajili ya kuipata dunia hii leo tunaona ni jinsi gani watoto wao wameathirika. Na zile familia zilizo ipa nyongo dunia, na kuvumilia dhiki zote kwa ajili ya dini hii leo tunaona ni jinsi gani watoto wao walivyostawi.
Dunia huwa yenye uharibifu pindi inapopupiwa na kisha dini kupuuzwa, kwa hivyo usiyajaribu haya. Amirul Muminin (a) ni yule ambaye ana tajruba kamili ya dini katika maisha yake na uzoefu wake unatosha kwetu.
Haya yalitokea katika zama zake na maswahaba wengi wakuu walishuhudia kwamba siku moja Mtume alitutahini kwa magumu na tukafanikiwa, lakini baadae tulipoipata dunia tuliiasi dini na hatimaye dunia yetu ikaangamia. Hii ni sheria ya Mwenyezi Mungu ambayo Amirul Mumin (a) anaisimulia hivi.
Anasema kwamba watu wakiasi dini kwa ajili ya dunia basi Mwenyezi Mungu huwafungulia mlango wa kuwaadhibu katika ulimwengu ule ule walioupupia kwa kuasi dini. Hii ni zawadi ya Amirul-Muminin (a) ambayo amewapa watu wa dini na waumini. Hupaswi kamwe kufanya mpango huu ili kusawazisha ulimwengu wako kwa malipo ya dini yako.
Kunapokuwa na uchaguzi kati ya dini na dunia. usiitoe dini. Kwani Unatakiwa uihifadhi dini yako kwa sababu katika mambo ya dunia kuna kupanda na kushuka. Tunaona kwamba siku moja dunia yetu huwa nzuri halafu hali ikawa mbaya zaidi, kisha tena ikawa nzuri. Lakini wale wanaoifanya dunia kuwa kusudi lao na kutoa fidia kwa dini zao basi ulimwengu wao huangamizwa.
Hivyo tunapaswa kushikilia kwa uthabiti na kushikamana na dini katika hali zote. Kwani hakuna kupanda na kushuka katika dini ambapo tunaweza kuiacha dini siku moja kwa ajili ya ulimwengu na kisha kurudi tena. Katika dini ukishaiacha dini huwa unabaki nje yake tu.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا مَنْ يَرْتَدَّ مِنْكُمْ عَنْ دِينِهِ فَسَوْفَ يَأْتِي اللَّهُ بِقَوْمٍ يُحِبُّهُمْ وَيُحِبُّونَهُ أَذِلَّةٍ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ أَعِزَّةٍ عَلَى الْكَافِرِينَ يُجَاهِدُونَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ وَلَا يَخَافُونَ لَوْمَةَ لَائِمٍ ۚ ذَٰلِكَ فَضْلُ اللَّهِ يُؤْتِيهِ مَنْ يَشَاءُ ۚ وَاللَّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ {54}
[5:54] Enyi mlio amini! Atakaye iacha miongoni mwenu Dini yake, basi Mwenyezi Mungu atakuja leta watu anao wapenda nao wanampenda, wanyenyekevu kwa Waumini na wenye nguvu juu ya makafiri, wanapigania Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawaogopi lawama ya anaye laumu. Hiyo ndiyo fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu na Mwenye kujua.
Katika Suratu Maida Allah s.w.t anasema kwamba mwenye kuacha dini Mwenyezi Mungu atamweka nje ya dini na kuleta umma mpya kwa ajili ya kusimamisha dini, na watakuwa ni watu ambao watapendwa na Mwenyezi Mungu nao pia watampenda Mwenyezi Mungu. Basi hawatachoka katika Njia ya Mwenyezi Mungu.
Sifa ya tatu ni kuwa wanyenyekevu kwa waumini na kua na ukali kwa makafiri. Kisha sifa nyingine ya wale wanaoiacha dini kwa ajili ya ulimwengu wao ni kwamba wakati umma mwingine utakapochukua mahali pao hawatamsikiliza yeyote anayewakemea na kuwahukumu kwa ajili ya dini. Mtu asiye kubali kuiacha dini kwa ajili ya dunia au familia au jamaa, na hata wateja huwashutumu, kuwakosoa, na kuwanyanyasa.
Lakini je kunapokuwa na ukosoaji kwa ajili ya udini basi tuache nini, dini?
La hasha tusiache dini hata kama dunia nzima itakusanyika kutukosoa. Basi watu wenye sifa ya kidini Hawajali isipokuwa wanatekeleza majukumu yao ya kidini.
Kutakuwa na panda shuka maishani. Leo hivi Mwenyezi Mungu amekupa mali, kisha kwa sababu fulani zikatoweka lakini kesho Mwenyezi Mungu anaweza kukupa tena. Lakini dini pindi ukiitelekeza basi mara moja utabaki nje na kuwa muasi.
Mwenye kuacha dini atambue kwamba litakuja kundi jengine badala yake. Kwa hivyo usifanye biashara hiyo ya kuifungia dini nje kwa ajili ya kupata maslahi machache ya dunia yako. Lau Watu watakulaani, kukukosoa na kukukejeli kwa jambo ambalo linakuchoma. Njia bora ni kutolitilia maanani, ikiwa unajua mimi basi hautakasirika endapo utakosolewa, basi ni bora uwape masikio japo kidogo pasi na kuzingatia hukumu zao bali endelea na kazi yako nao watachoka.
Ninayasema haya katika nuru ya Hadith kwamba ikiwa utasimamisha dini basi dunia yako pia itaimarika. Ukiitanguliza dunia yako kwa kuasi dini yako basi dunia uliyoipupia na dini uliyoipuuza zote zitaangamizwa. Usiifanye dini iwe ni kwa ajili ya kupata baraka tu bali ifanye kuwa ni sera ya maisha yako na iwe ni dalili ya kutosha kwetu kwamba Amirul-Muminin (a) anasema hivyo na kwa hakika aliifanya dini kuwa kama sera ya maisha. Alipewa utawala, na mamlaka kuwekwa chini ya nyayo zake. Moja wapo ni pale Mwenyezi Mungu alipo mpa utawala huko Ghadir, lakini watu pia waliweka uongozi mara kadhaa miguuni pake.
Mfano katika Shura iliyoandaliwa na Khalifa wa pili, ili kuteua mrithi wake. Mkutano ulipoanza Zubair alisema kura yangu iko kwa Ali, kisha wengine nao wakasema kura yangu pia iko kwa Ali lakini kwa masharti na kisha kura ya mwisho ambayo ilikuwa ya Abdur Rahman ibn Awf aliyekuwa mkuu wa shura ya kuamua alitoa nafasi hiyo kwa masharti lakini Ali hakufanya makubaliano naye. Jambo ambalo sisi tunalifanya kwa urahisi.
Imam Ali katika shura hii alikuwa hapati biashara bali utawala wa usultani ulioenea katika mabara matatu. Lakini kwa kuwa masharti aliyopewa hayakukubaliana na dini aliepukana nayo. Kisha baada ya kuuawa kwa Khalifa wa tatu watu walipokuja na akasema walikuja kwa haraka kwa wingi kiasi kwamba Hasan na Husein ambao walikuwa vijana lakini walikuwa wakikandamizwa.
Alisema, ningeweka tawala za Khalifa mahali pale pale palipokuwa hapo awali lakini pindi watu walipokuja uthibitisho ulitimia na ilinibidi kulikubali hili kama jukumu la kiungu. Anasema katika msemo wake maarufu utawala huu hauna thamani kwangu ikiwa siwezi kuanzisha haki kupitia utawala huo.
Kwa kweli tunapaswa kujifahari juu ya Imamu wetu huyu na angalau kiwango japo kidogo cha tabia yake kinapaswa kuonekana katika maisha yetu. Tusijaribu kuwafurahisha Maimamu wetu kwa namna yetu ya kuimba na kucheza kwa kauli mbiu zao. Bali tumfurahishe Amirul-Muminin (a) kwa kufuata mienendo yake.
Tukikumbuka kanuni mojawapo aliyoiweka yeye ni kwamba, kamwe usikubali kuachana na dini yako kwa ajili ya dunia, hivyo hatimaye utaipoteza dunia yako na vilevile akhera yako .