Watu wa familia ya Shireen Abu Akleh, mwandishi habari Mpalestina ambaye aliuliwa shahidi kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel akiripoti matukio yaliyokuwa yakijiri katika mji wa Jenin, wamokosoa vikali ripoti iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani kuhusu mauaji hayo.
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani imetangaza matokeo ya uchunguzi kuhusu risasi iliyomuuwa mwandishi huyo wa habari aliyekuwa akifanyia kazi televisheni ya al Jazeera ya Qatar na kudai kuwa: Kutokana na kuvunjika vunjika kwa risasi hiyo haiwezekani kutoa tathmini sahihi kuhusu mauaji hayo!
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani huku ikitegemea ripoti ya timu ya uchunguzi imetangaza kuwa, upo uwezekano kwamba risasi iliyomuuwa Shireen Abu Akleh ni kati ya silaha za wanajeshi wa Israel, hata hivyo imesema kuwa hakuna kiashiria kinachoonyesha kuwa wanajeshi wa Israel walimfyatulia risasi kwa makusudi mwandishi huyo wa habari wa Mpalestina.
Mtandao wa habari wa Shahab leo umeripoti kuwa, Tony Abu Akleh, kaka yake Shireen Abu Akleh amesisitiza kwamba: Matokeo yaliyotangazwa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani kimsingi hayakubaliki.
Tony Abu Akleh ameongeza kuwa: “Suala hili liko wazi kikamilifu kwamba wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel, katika tukio hilo la mauaji, walimfyatulia risasi 16 mwandishi huyo wa habari wa Kipalestina na moja ndiyo iliyomuuwa, na nyingine ilimjeruhi ripota mwingine wa Kipalestina.”
Wakati huo huo viongozi wa Palestina wameituhumu serikali ya Marekani kuwa imefanya kila iwezalo kuukingia kifua utawala ghasibu wa Israel katika jinai hiyo.
Shireen Abu Akleh aliyekuwa na umri wa miaka 51, ripota wa televisheni ya al Jazeera yenye makao yake nchini Qatar, aliuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa utawala haramu wa Israel tarehe 11 mwezi Mei mwaka huu wakati akiripoti uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika Msikiti wa al Aqsa.