Dar es Salaam. Wakati baadhi ya viongozi wastaafu wakitupiwa lawama ya kuacha kuandika historia halisi ya nchi, Balozi wa zamani Ami Mpungwe amevunja ukimya kwa kueleza ugumu wa sheria za Tanzania katika kufanikisha hilo.
Amesema zipo changamoto iwapo utataka kuandika historia ya yaliyotokea nchini, akitaja ugumu wa upatikanaji wa nyaraka muhimu za kihistoria.
Balozi Mpungwe ameyasema hayo jana, Julai 6, 2022 alipokuwa anajibu swali la mmoja wa wanafunzi kuhusu kukosekana kwa historia, wakati wa mdahalo wa mchango wa Kiswahili katika Ukombozi wa Afrika.
“Ni jambo la msingi, mimi binafsi naona kama nina deni. Kuna mambo fulani fulani… sio mengi nayajua ambayo Tanzania imeyafanya lakini naweza kuondokana nayo na baadaye watafiti watateseka,” amesema.
Ameeleza ugumu uliopo katika upatikanaji wa nyaraka kutoka Serikali kuhusu historia hizo, unasababisha watu kutoka mataifa mengine waiandike historia ya Tanzania kwa tafsiri zao.
“Mimi binafsi naandika kuhusu tulichokifanya Arusha kuwasaidia Wanyarwanda, lakini nikiomba nyaraka serikalini kwetu sina uwezo wa kupata na karatasi nyingi niliandika mimi mwenyewe lakini leo siwezi kuzipata,” amesema.
Kulingana na balozi huyo, kuna wakati alipata nyaraka kutoka Serikali ya Marekani kuhusu anachotaka kuandika, ambazo ziliandikwa kinyume.
Amebainisha kuwa sababu ya kuhitaji nyaraka hizo ni kupata uhakika wa baadhi ya matukio zikiwemo tarehe, majina ya watu, na kukosekana kwake kunasababisha iandikwe historia isiyokamilika.
Ameitaka Serikali kurahisisha mazingira ya upatikanaji wa nyaraka hizo, huku akiitahadharisha kuzuia zile zinazoonekana kuwa na hatari kwa maslahi ya taifa.