Iran, Russia na China kushiriki katika mazoezi ya kijeshi Amerika ya Kusini

Iran, Russia na China zinapanga kushiriki katika mazoezi ya kijeshi yatakayoandaliwa na Venezuela ili kuonyesho nguvu zao kwa Marekani.

Maneva hayo ya kijeshi yanafuatia yale yaliyoandaliwa na Iran yakishirikisha majeshi ya majini ya China na Russia kwa anwani ya “Ukanda wa Amani wa Baharini 2022” katika eneo la kaskazini mwa Bahari ya Hindi.

Mazoezi mbalimbali ya kimbinu ikiwa ni pamoja na kuokoa chombo kinachoungua, kukomboa chombo kilichotekwa nyara, ufyatuaji risasi dhidi ya shabaha mahususi, ufyatuaji risasi usiku kwenye shabaha zilizoko angani na mazoezi mengine ya kimbinu na kiutendaji yalifanyika katika maneva hayo.

Kwa mujibu wa tovuti ya Washington Free Beacon, Iran, Russia na China zinapanga kushiriki katika mazoezi ya kijeshi huko America ya Latini  yatakayopewa jina la “Sniper Frontier” ili kuonyesha nguvu zao kwa Marekani.

Venezuela ndiyo mwenyeji wa mazoezi hayo ya kijeshi ambayo yamepangwa kufanyika mapema mwezi wa Agosti, na majeshi ya Iran, Russia, na China yanapanga kwenda Amerika ya Latini na Caribbean kushiriki katika maneva hayo.

Washington Free Beacon imeandika kuwa, mazoezi haya ya kijeshi ni moja ya dalili za wazi za kuundwa muungano dhidi ya Marekani katika eneo la Amerika ya Kusini.

Mchambuzi wa masuala ya usalama wa taifa, Joseph Humire ameuambia mtandao wa Washington Free Beacon kwamba Russia na washirika wake yaani Iran na China, wako katika harakati za kuonyesha nguvu kubwa kwa kushiriki katika mazoezi haya ya kijeshi nchini Venezuela.”

Vyombo vya habari vya Marekani vimesema mazoezi ya majini kati ya Iran, Russia na China yanatuma ujumbe mzito kwa Marekani.

Gazeti la Washington Times limeandika kuwa mazoezi hayo ya pamoja ya wanamaji wa Iran, Russia na China ndiyo makubwa zaidi kuwahi kuhusisha meli za kivita za nchi hizo tatu na ya kwanza tangu Iran ilipoalikwa rasmi kujiunga na mkataba wa usalama wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai (SCO) mwezi Septemba mwaka jana.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *