Waziri Mkuu wa muda wa utawala haramu wa Israeli, Yair Lapid, ametoa amri ya kufungwa kwa ubalozi wa utawala huo nchini Eritrea baada ya viongozi wa nchi hiyo ya Mashariki mwa Afrika kukataa kumpokea balozi mpya wa utawala huo haramu kwa miaka miwili sasa.
Katika miaka ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umeweka ajenda ya kuanzisha na kupanua uhusiano na nchi za Kiarabu na Kiafrika. Katika mkondo huo, nchi mbili za Kiarabu yaani Imarati na Bahrain, na Sudan na Morocco zikiwa nchi za Kiafrika zimeanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni katika miaka ya karibuni. Miongoni mwa malengo makuu ya hatua ya utawala wa Kizayuni katika kuanzisha na kustawisha uhusiano na nchi hizo, ni kutaka kujiondoa katika hali ya kutengwa kisiasa katika eneo la Magharibi mwa Asia, na pia kutumia fursa ya kuwa na uhusiano na nchi za Kiafrika kwa ajili ya kuzishawishi nchi za Asia Magharibi kurekebisha uhusiano na utawala huo.
Suala la kuanzisha na kuendeleza uhusiano wa nchi mbalimbali za Kiarabu na Kiafrika na utawala wa Kizayuni wa Israel linapingwa na watu wengi ndani ya nchi zinazolengwa. Bahrain ni moja kati ya nchi ambazo zimekuwa zikishuhudia maandamano ya mara kwa mara ya wananchi wanaopinga hatua ya utawala wa Manama ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni, na upinzani huo unaongezeka siku baada ya nyingine. Hata hivyo, kwa kuzingatia kwamba utawala wa ukoo wa Aal-Khalifa ni utawala tegemezi kwa Saudia na Marekani, na pia unakabiliwa na mgogoro wa uhalali ndani ya Bahrain kwenyewe, umekuwa ukipuuza maandamano ya wananchi na kutumia mahusiano hayo kusalia madarakani.
Hata hivyo, muqawama na mapambano ndio suluhisho linaloweza kuutia adabu utawala wa Kizayuni wa Israel. Kwa mfano tu, makundi ya muqawama ya Lebanon na Palestina yamefichua udhaifu wa kijasusi, kiusalama na kijeshi wa utawala wa Kizayuni na kudhihirisha kuwa ngano za kutoshindwa jeshi la Israel hazina msingi wowote. Jambo jingine muhimu sana katika uwanja huo ni kwamba upinzani na kusimama kidete wananchi kumezuia au kuzorotesha uhusiano wa utawala wa Kizayuni na nchi nyingine. Mfano hai wa ukweli huu ni Misri ya mwaka 2011. Wakati huo, wananchi wa Misri sambamba na kupinga uhusiano wa nchi hiyo na utawala wa Kizayuni, walishambulia ubalozi wa Israel mjini Cairo, na balozi wa utawala huo akatoroka mjini Cairo nyakati za usiku.
Sasa muqawama wa wananchi na serikali ya nchi ya Kiafrika ya Eritrea umemlazimisha Yair Lapid, Waziri Mkuu wa muda wa utawala wa Kizayuni wa Israel, aamuru kufungwa ubalozi wa utawala huo mjini Asmara, baada ya Eritrea kukataa kumpokea balozi wa utawala huo kwa kipindi cha miaka miwili. Balozi wa mwisho wa Israeli aliondoka Asmara mnamo Septemba 2018, na tangu wakati huo hakuna balozi yeyote mwingine wa utawala huo aliyekubaliwa na Eritrea. Kufungwa ubalozi wa Israel mjini Asmara ni pigo jingine kwa utawala huo ambao unapingwa na Waafrika waliowengi kutokana na sera zake za kukoloni ardhi za Palestina.
Itmar Eichner, mwandishi wa safu ya siasa wa gazeti la Israel la Yedioth Aharonot, hapo awali aliandika katika ripoti kwamba: “Hadi Aprili 2020, afisa wa usalama wa ubalozi ndiye aliyekuwa mwakilishi pekee wa Israeli nchini Eritrea; na katika upande wa kisiasa, hakuna ndege iliyotua kwenye uwanja wa ndege wa Ben Gurion kwa muda mrefu ikiwa imebeba maafisa wakuu wa Eritrea. Israel ina milki tatu zilizo wazi katika nchi hiyo ya Afrika ambazo ni ofisi ya ubalozi, makazi ya balozi na makazi ya dereva. Katika ubalozi huo, kuna wafanyakazi wa ndani, wakiwemo walinzi, ambao wengi wao, isipokuwa walinzi wachache, wamekaa majumbani mwao.”
Tukifumbia jicho sababu halisi za upinzani wa serikali na wananchi wa Eritrea dhidi ya utawala wa Kizayuni Israel, inatupasa kusema kuwa, kufungwa ubalozi wa utawala huo nchini Eritrea kunahatarisha maslahi yaIsrael katika eneo la Pembe ya Afrika. Wakati huo huo, mwenendo huu wa Eritrea unaweza kuwa kielelezo na mfano wa kuigwa na nchi na mataifa mengine ili kuzuia njama za kuanzishwa uhusiano wa serikali zao na utawala wa Kizayuni kupitia upinzani na mapambano.