Wabunge hawa ni moja wapo wa Wanasiasa wa Tanzania waliopinga na kukerwa na kuanzishwa upya kwa uhusiano wa Tanzania na Utawala haramu wa Israel.
Dodoma. Safari chache za nje ya nchi zilizofanywa na Rais John Magufuli tangu aingie madarakani na uhusiano wa kimataifa wa Tanzania na nchi kadhaa, ni baadhi ya mambo yaliyogusa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya mwaka 2018/19.
Wakati mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ akijikita kujadili safari za Rais, Zitto Kabwe (ACT- Wazalendo Kigoma Mjini) alikosoa uhusiano wa Tanzania na nchi kadhaa zikiwemo Morocco na Israel, hoja ambayo pia ilijadiliwa na wabunge kadhaa. Akizungumza katika mjadala wa bajeti hiyo iliyojadiliwa na kupitishwa kwa siku moja jana mchana, Sugu alisema suala la Rais Magufuli kusafiri nje ya nchi haliepukiki, na kwamba kuna mikutano inayopaswa kuhudhuriwa na Rais mwenyewe na siyo kuwakilishwa na Makamu wa Rais au Waziri Mkuu.
Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli ametembelea nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na Ethiopia huku akitimiza takriban miaka miwili na nusu tangu aapishwe Novemba 5, 2015. Machi mwaka huu, kiongozi huyo mkuu wa nchi alizungumzia safari zake akisema hakuchaguliwa na Watanzania ili kusafiri nje ya nchi.
Alitoa kauli hiyo akiwa mjini Singida katika uzinduzi wa kiwanda cha mafuta ya kupikia cha Mount Meru Millers Group na akabainisha kuwa amekataa zaidi ya mialiko 70 ya nchi mbalimbali ili kuwatumikia Watanzania.
Rais alisema jimbo lake ni Tanzania na hawezi kwenda nje wakati hajamaliza kutatua kero za wananchi waliompigia kura.
“Suala la kusafiri bado ni muhimu, tena anapokwenda nje anaweza kutumia lugha ya Kiswahili kwa sababu Rais Xi Jinping wa China kila anapokwenda anaongea Kichina licha ya kuwa msomi na anazungumza Kiingereza,” alisema Sugu.
“Kama tatizo ni gharama, mbona anatuma delegation (ujumbe) mara Makamu wa Rais, mara Waziri Mkuu nao wanatumia gharama kwa sababu hawaendi kule kwa miguu.”
Sugu ambaye hivi karibuni alitoka gerezani kwa msamaha wa Rais alisema, “mikutano ya Commonwealth (Jumuiya ya Madola) ni ya wakuu wa nchi, lakini sisi tunatuma wawakilishi, kuna fursa za kiuchumi na kibiashara.”
“Rais Uhuru Kenyatta (wa Kenya) ametumia vizuri sana fursa za uchumi na kibiashara kwa nchi yake alivyokwenda pale (kwenye mkutano wa Commonweath – Uingereza, mwaka huu) hali kadhalika Rais wa Afrika Kusini naye anatumia fursa.”
Alisema kutokana na fursa hizo, Rais kusafiri nje hakuepukiki. “Ni kama alivyonukuliwa mzee Kikwete (Jakaya-Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne) aliposema kusafiri kumemsaidia sana kwani mkaa bure si sawa na mtembea bure,” alisema mbunge huyo.
Kwa upande wake, Zitto alipinga Tanzania kufungua ubalozi Israel na kurudisha uhusiano na Morocco kwa maelezo kuwa nchi hizo zimekuwa zikikandamiza nchi nyingine.
Wakichangia bajeti hiyo, wabunge walisema msimamo wa Tanzania kuhusu mgogoro wa Israel na Palestina unaelezwa vizuri katika nukuu ya Mwalimu Julius Nyerere aliyoitoa mwaka 1967.
Zitto alisema msimamo huo ndio umekuwa msingi wa sera ya mambo ya nje ya Tanzania kwa miaka mingi kabla ya utawala wa sasa.
Alisema kitendo cha Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga kuonekana akinywa mvinyo na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu wakati wananchi wa Palestina wakiuawa kimemtia aibu kwa madai kuwa Israel imekuwa ikiwaumiza Wapalestina.
“Nchi inaona aibu kulaani mauaji ya wanyonge walionyang’anywa nchi yao. Umeonekana (Dk Mahiga) katika televisheni ya Israel ukizungumza bila kusema lolote kuhusu wanyonge (Palestina), ulikuwa unavunja heshima,” alisema Zitto.
Hoja hiyo ya Zitto, pia ilizungumzwa na Sugu aliyesema, “Mwalimu Nyerere alifuta urafiki wa kibalozi kwa Israel kutafuta uhuru, tujiulize tunakwenda kufungua ubalozi Israel? Mwalimu Nyerere na sisi kama Taifa tulifuta urafiki na Morocco, lakini leo tumeacha sera zetu dhidi ya Morocco kwa ahadi ya kujengewa uwanja wa mpira, tunajivunjia heshima kwa ahadi ya kujenga uwanja wa mpira?”