Maseneta waitaka serikali ya Biden kuwajibika kuhusu uchunguzi wa mauaji ya Shireen

Maseneta wa chama cha Democratic cha Marekani wameitaka serikali ya Rais Joe Biden wa nchi hiyo kuwajibika kuhusu uchunguzi unaohusu mauaji ya mwandishi wa habari wa Palestina wa televisheni ya Al Jazeera, Shireen Abu Akleh.

Ni baada ya Umoja wa Mataifa kumesema kuwa taarifa ulizokusanya zinaonesha kuwa, Shireen Abu Akleh, mwandishi wa habari wa televisheni ya al-Jazeera ya Qatar, aliuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Israel.

Kundi la Maseneta wa chama cha Democratic wa Marekani, akiwemo Chris Van Hollen, Patrick Leahy, Chris Murphy na Dick Durbin limemwandikia barua Anthony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, likiutaka utawala wa Rais Joe Biden kujibu uchunguzi kuhusu mauaji ya mwandishi wa habari wa Palestina Shireen Abu Akleh likisema kuwa uchunguzi uliofaywa na serikali ya Marekani kuhusu kadhia hiyo haukuwa huru.

Takwa hili la maseneta wa chama cha Democratic nchini Marekani lilitolewa saa chache kabla ya safari ya Joe Biden katika eneo la Asia Magharibi siku ya leo Jumatano.

Maseneta wa chama cha Democratic na maseneta wengine 20, pamoja na wajumbe 57 wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, awali walikuwa wameiomba serikali ya nchi hiyo kufanya uchunguzi huru kuhusu mauaji ya Shireen Abu Akleh.

Baada ya jinai hiyo iliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel kumetolewa miito mingi inayoitaka Marekani iangalie upya sera zake za kuuunga mkono bila ya masharti utawala wa Kizayuni na kusitisha misaada yake ya kila mwaka kwa utawala huo.

Nchi, taasisi na mashirika mengi ya kimataifa yamelaani jinai hiyo ya Wazayuni na kutaka utawala wa Kizayuni wa Israel uwajibishwe kwa ukatili huo.

Mapema mwezi uliopita wa Mei mwandishi wa habari ya televisheni ya Al Jazeera, Shireen Abu Akleh, 51, alipigwa risasi kichwani na kuuliwa kikatili na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wakati akiwa kwenye kazi yake ya kuripoti uvamizi wa kijeshi wa jeshi la Israel katika kambi ya wakimbizi wa Palestina ya Jenin.

Uchunguzi mpya wa gazeti la Marekani la New York Times umethibitisha kuwa risasi iliyomuua mwandishi wa habari wa televisheni ya Al Jazeera ya Qatar, Shireen Abu Akleh, ilifyatuliwa na mwanajeshi wa kikosi maalumu cha Israel, katika eneo ambalo halikuwa na mwanamgambo hata mmoja wa Kipalestina.

Hadi sasa jeshi la Israel limekamata, kujeruhi au kuwauwa shahidi mamia ya waandishi wa habari.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *