Sonko aruhusiwa Kuwania Ugavana wa Mombasa, Presha kwa Abdulswamad Shariff Nassir

FARAAN:Majaji watatu wa Mahakama Kuu mnamo siku ya Jumatano tarehe 13 July 2022 walimruhusu aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Mike Sonko kuwania wadhifa huo Mombasa, hatua inayotarajiwa kumtia presha mwaniaji wa ODM Abdulswamad Shariff Nassir.

Bw. Nassir amekuwa kifua mbele kwenye azma ya kumrithi Gavana Ali Hassan Joho, lakini hatua ya majaji Olga Sewe, Stephen Githinji na Anne Ong’injo sasa itabadili hesabu zake.

Jopo la majaji hao liliamuaru Msimamizi wa uchaguzi katika Kaunti ya Mombasa, Bi Swalha Ibrahim, akubali stakabadhi za uteuzi alizowasilisha Bw Sonko.

Lilitoa pia uamuzi kuwa, Bw Sonko anaruhusiwa kuwania ugavana baada ya kukubali maombi yake kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) isiruhusiwe kumzuia.

Bw Sonko pia alikuwa ametaka uamuzi uliotolewa na kamati ya kusikiliuza na kutatua mizozo ya uchaguzi (DRC) kumzuia kuwania ugavana wa Mombasa, utupiliwe mbali.

Mahakama hiyo pia ilitoa uamuzi kuwa IEBC ilikuwa imevunja kifungu cha tatu cha katiba pamoja na vifungu vya 10, 47, 49 na 59.

Mahakama ilinukuu kuwa, IEBC ilienda kinyume na katiba kwa kumzuia Bw Sonko kugombea, ilhali kesi yake haikuwa imetatuliwa katika mahakama ya juu.

“Ni maoni yetu kuwa, IEBC ilimzuia Bw Sonko bila sababu ya kisheria, licha ya kujua ana kesi katika Mahakama ya Juu,” walieleza majaji.

Walieleza kuwa IEBC haiwezi kupuuza Mahakama ya Juu, wakati ambapo ni washtakiwa katika kesi ya kubanduliwa kazini.

“Bi Ibrahim alimnyima haki ya kikatiba Bw Sonko kwa kukataa kupokea shahada yake,” walisema mahakimu hao.

Kulingana na mahakama hiyo, IEBC haikuwa na sababu ya kukataa kumuidhinisha Bw Sonko kuwania ugavana.

Mahakama pia ilieleza kuwa gavana huyo wa zamani wa Nairobi alikuwa amewasilisha stakabadhi zote zilizoitishwa na Bi Ibrahim, ikiwemo shahada iliyothibitishwa, ambayo Bw Sonko aliweka juhudi kuhakikisha imemfikia.

Jopo hilo lilielezea kuwa, shahada aliyowasilisha Bw Sonko ilikuwa ya chuo kikuu cha humu nchini na haikuhitaji kuthibitishwa na Tume ya kusimamia Masomo ya Juu (CUE).

Bw Sonko pamoja na chama cha Wiper, waliipongeza mahakama kwa uamuzi huo wakidai kuwa umewapa matumaini watu wa Mombasa.

Mwongozo

Mawakili wa IEBC wakiongozwa na Bw Edwin Mukele walieleza mahakama kuwa, watasubiri mwongozo kutoka kwa tume hiyo ya uchaguzi.

Kulingana nao IEBC ina wajibu wa kuiheshimu mahakama.

Wakili wa Bw Sonko – George Khaminwa – alitaka IEBC ieleze kwanini mnamo 2017 walimruhusu Bw Sonko kuwania ugavana na shahada yake na kisha kubadili msimamo 2022.

Wakati uo huo mawakili wa Bw Sonko walikuwa wamewasilisha maombi Jumanne dhidi ya Mwenyekiti wa IEBC Bw Wafula Chebukati, kwa kukiuka maagizo ya mahakama yaliyotolewa manmo Julai 4.

Maombi hayo yalitaka IEBC izuiwe kuchapisha majina ya wagombea wa kiti cha ugavana kaunti ya Mombasa.

Mahakama iliitaka IEBC itume majibu yake na kesi hiyo itajwe Julai 18.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *