Kundi moja la kutetea haki za binadamu limeutaka Umoja wa Mataifa kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel usitishe sera za kutumia mabavu ambayo hupelekea idadi kubwa ya Wapalestina kupoteza maisha.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Euro-Med Monitor limemtumia barua Morris Tidball-Binz, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji nje ya mkondo wa sheria au mauaji ya kiholele na kusema, “Maagizo rasmi yaliyopokelewa na jeshi la Israel katika kukabiliana na raia wa Palestina yalisababisha matumizi ya kimfumo ya nguvu zinazosababisha mauaji, na hivyo kusababisha ongezeko kubwa la matukio ya mauaji ya kiholela katika maeneo ya Palestina.”
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, jeshi la utawala haramu wa Israel limewaua karibu Wapalestina 53 katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na al-Quds (Jerusalem) Mashariki, kutokana na sera ya utumiaji nguvu kupita kiasi dhidi ya Wapalestina, barua hiyo imesema.
Wanajeshi wa Israel wanatumia nguvu kuua kimakusudi Wapalestina, barua hiyo imeongeza, ikinukuu mauaji ya Rafiq Riyad Ghannam huko Jenin wiki iliyopita.
Jumatano iliyopita, vikosi vya Israel vilivamia makazi ya Wapalestina mashariki mwa mji wa Jaba’ huko Jenin, kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, na kumuua Ghannam, 21, ambaye alitoka nje ya nyumba yake akiwa amevalia nguo za kulala baada ya kusikia sauti isiyo ya kawaida nje.
Tukio hilo la ufyatuaji risasi linaonyesha sera ya Israeli ya kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia wasio na silaha ambao, mara nyingi, sio hatari inayohitaji matumizi ya risasi.
Kulingana na kundi hilo la haki za binadamu, sera ya jeshi la Israel ya kufyatua risasi tayari ilikuwa dhaifu huko nyuma na mara nyingi ilisababisha mauaji ya kiholela bila uhalali. Kupitishwa kwa sera mpya ya ufyatuaji risasi mapema mwaka 2021, kulifanya hali ya mambo kuwa mbaya zaidi ambapo wanajeshi wa utawala katili wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wamepata idhini rasmi ya kuwafyatulia risasi Wapalestina wanaorusha mawe.
Barua hiyo ilimtaka Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa na vyombo vingine husika kufuatilia na kuchunguza mauaji ya raia wa Palestina, kuwalinda na kuchukua hatua za dhati kuhakikisha uwajibikaji kuhusu mauaji ya kiholela.