Kukiri wataalamu wa Kizayuni kuwa uwezo wa nyuklia wa Iran hauwezi kuharibiwa kijeshi

Katika kujibu maneno ya Dakta Kamal Kharrazi Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Iran na Mkuu wa Baraza la Kistratejia la Sera za Kigeni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mkuu wa Majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel amezungumzia kile amekitaja kuwa tishio la Iran na chaguo la kijeshi na kusema chaguo la kijeshi dhidi ya Iran ni jukumu la kimaadili tu.

Katika mahojiano na Televisheni ya Al Jazeera ya Qatar, Dk Kharrazi alisema Iran ina uwezo wa kiufundi wa kuunda bomu la atomiki, lakini haina nia ya kuliunda.

Ukweli ni kuwa, utawala haramu wa Israel hauwezi kuzungumzia maadili kwa sababu umekiuka misingi na vigezo vyote vya kimaadili. Utawala wa Israel unapinga haki ya mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani wakati yenyewe, tangu mwanzo wa kukalia kwa mabavu Palestina imefanya juhudi zote za kupata silaha za nyuklia.

Israel ilianza kufuatilia malengo ya kijeshi katika sekta ya nyuklia mapema muongo wa 60, na kinyume na sera yake iliyotangazwa kwamba kufikiwa kwa uwezo kama huo kulionekana kama hitajio lisiloepukika la kuunda kizuizi dhidi ya nchi za Kiarabu, uwezo huo wa silaha za nyuklia ulitumika katika kufikia malengo haramu ya kujipanua utawala huo. Utawala wa Kizayuni wa Israel umekiuka ahadi zake za kimataifa, na unaendelea kupuuza mikataba na maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Utawala huo dhalimu umekataa kutia saini mapatano ya kuzuia usambazaji wa silaha za  nyuklia, NPT ili kukwepa vikwazo katika mipango yake ya kuzalisha na kujirundikia silaha hizo hatari. Aidha utawala huo umekataa ukaguzi wa kimataifa ufanyike katika vituo vyake vya nyuklia.

Ili kuwa na ukiritimba wa nguvu za nyuklia, utawala wa Kizayuni haujaruhusu nchi yoyote ya Kiarabu, hata Misri, ambayo imetia saini mkataba wa amani na utawala huo, kupata nguvu ya nyuklia hata kwa malengo ya amani, na mbali na hayo imeshambulia pia vituo vya nyuklia vya  nchi za Iraq na Syria.

Lakini mbinu hiyo ya Israel  haijawa na ufanisi kwa Iran hadi sasa kwa sababu uwezo wa nyuklia wa Iran ni mkubwa mno na wataalamu wote wamefikia natija kwamba haiwezekani kuharibu nguvu za nyuklia za Iran kwa hujuma za kijeshi, na wakati wa urais wa Obama, Marekani na nchi nyingine za Magharibi ziliamua kufikia makubaliano ya nyuklia na Iran yanayojulikana kama JCPOA. Mapatano hayo yalifikiwa na nchi za Magharibi baada ya kubainika kwamba hakuna uwezekano wa kuharibu nguvu za nyuklia za Iran kutokana na kuwa Iran imetegemea uwezo wa wataalamu wake wa ndani na hivyo hata taasisi zake za nyuklia zikilengwa itaweza kuzijenga upya bila msaada wa kigeni.

Hata kama wakati huo, kuna baadhi ya watu waliodhani kwamba kwa kutumia nguvu na vikwazo vya juu zaidi, wangeweza kupata matokeo bora dhidi ya Iran, lakini sasa wanakiri wazi kushindwa kwa dhana hiyo. Kwa msingi huo, utawala wa Kizayuni, kinyume na madai yake, hauwezi kuharibu vituo vya nyuklia vya Iran kama ilivyofanya huko Iraq kupitia mashambulizi ya kushtukiza, wala hauwezi kustahimili shambulio kutoka Iran kwa sababu ya udhaifu wake.

Ijapokuwa Iran hivi sasa haina bomu la atomiki na wala haina nia ya kuliunda, lakini ina makombora yenye nguvu na ndege zisizo na rubani na lengo la kumiliki zana hizo ni kuwa na uwezo wa kumzuia adui kuanzisha mashambulizi.

Kwa hakika, iwapo utawala wa Kizayuni wa Israel utathubutu kuchukua hatua zozote za kijeshi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, basi utawala huo utakumbwa na mashambulizi makubwa ya makombora yanayolenga shabaha kwa ustadi kote Israel. Kwa msingi huo baadhi ya wataalamu wa masuala ya kijeshi wanasema kuwa, bomu la atomiki la Iran litakuwa ni kituo cha nyuklia cha Israel katika eneo la Dimona kwani kikilengwa kitausababishia maafa makubwa utawala wa Kizayuni. Hata hivyo, hatupaswi kupuuza ukweli kwamba kutokana na safari ya Rais Joe Biden wa Marekani huko Tel Aviv, vitisho vya kieneo vya utawala wa Kizayuni vimeongezeka.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *