Matokeo ya utafiti uliofanywa katika majimbo mbalimbali ya Marekani yanaonyesha kuwa, vitendo na mienendo ya ubaguzi wa rangi dhidi ya raia wa nchi hiyo wenye asili ya Asia imeongezeka katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian, matokeo ya utafiti uliofanywa katika majimbo tofauti ya Marekani na kituo cha binafsi kinachoshughulikia haki za raia wenye asili ya Asia (AAPI) yanaonyesha kuwa, vitendo na miamala ya kibaguzi dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Asia iliongezeka baina ya mwaka 2020 na 2022 kutokana matatizo ya kiuchumi na kimaisha na msambao wa virusi vya corona nchini humo.
Utafiti huo umeonyesha kuwa, kuna matukio zaidi ya elfu tisa ya vitendo na miamala ya ubaguzi wa rangi iliyosajiliwa nchini Marekani waliyofanyiwa raia wenye asili ya Asia.
Kwa mujibu wa kituo cha binafsi kinachoshughulikia haki za raia wenye asili ya Asia (AAPI), katika kipindi hicho cha miaka miwili, mienendo na vitendo vya ubaguzi wa rangi dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Asia viliongezeka kwa asilimia 339, ambapo takribani khumsi moja ya raia hao walikumbwa na vitendo hivyo.
Katika miaka ya karibuni, na hasa wakati wa utawala wa Donald Trump, mitazamo ya ubaguzi wa rangi na ya mrengo wa kulia aliyokuwa nayo kiongozi huyo imechangia kushamiri ubaguzi wa rangi na vitendo vya ukatili vinavyosababishwa na chuki za ubaguzi nchini Marekani. Trump alikuwa mmoja wa waungaji mkono wakubwa wa mavuguvugu ya wazungu wanaojiona bora, kiasi kwamba alishawahi mara kadhaa kuyakosoa makundi yanayopiga vita ubaguzi wa rangi likiwemo la Maisha ya Watu Weusi Yana Thamani.