Iran yavunja mtandao wa majasusi wa Mossad ya Israel

Wizara ya Intelijensia ya Iran imetangaza habari ya kutiwa mbaroni majasusi kadhaa waliokuwa wakitumikia shirika la ujasusi la Israel (Mossad).

Taarifa ya wizara hiyo imeeleza kuwa, vyombo vya usalama vya Jamhuri ya Kiislamu vimewatia nguvuni majasusi hao waliojipenyeza nchini kupitia eneo la Kurdistan, magharibi mwa Iran.

Kwa mujibu wa Wizara ya Intelijensia ya Iran, maajenti hao wa utawala wa Kizayuni wa Israel walikuwa wametumwa hapa nchini kufanya mashambulizi ya kigaidi, sambamba na kuvamia maeneo nyeti ya taifa hili.

Hata hivyo Wizara ya Intelijensia ya Iran imesema majasusi hao wa Mossad ya Israel wametiwa mbaroni kabla ya kutekeleza jinai hizo, kutokana na kuwa macho vyombo vya usalama vya taifa hili.

Taarifa ya wizara hiyo imeeleza kuwa, majasusi hao wa utawala haramu wa Israel walikuwa na suhula na vyombo vya kisasa kabisa vya mawasiliano na mada za miripuko. Iran imefanikiwa kutwaa silaha hizo za maadui.

Ikumbukwe kuwa, Aprili 20 mwaka huu, Wizara ya Intelijensia ya Iran ilitangaza kukamatwa kwa majasusi watatu wa Mossad huko Sistan na Baluchistan.

Aidha maafisa wa usalama Iran mwezi Machi pia walisambaratisha makundi mawili ya magaidi wanaopata himaya ya kigeni ambao walikuwa wanalenga kuwaua raia wa kigeni wanaofanya kazi katika miradi ya maendeleo katika mkoa wa Sistan na Baluchestan.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *