Jenerali Hajizadeh: Karibuni hivi roketi la kubebea satalaiti la Qaem litakuwa tayari kutumwa angani

Kamanda wa kikosi cha anga za mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema roketi la kubebea satalaiti la Qaem karibuni hivi litakuwa tayari kurushwa kwa ajili ya kutumwa katika anga za mbali.

Katika miaka miwili iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejikita katika uundaji maroketi ya kubebea satalaiti na kuweza kupiga hatua muhimu katika urushaji wa satalaiti; na kwa kufanya hivyo kupanua wigo wa uundaji maroketi ya kubebea satalaiti sambamba na utengenezaji wa satalaiti zenyewe.

Hivi sasa wataalamu wa Kiirani wameweza kuwa na utaalamu kamili wa teknolojia ya anga za mbali, yaani utaalamu wa kujenga vituo vya kurushia maroketi, mitambo ya urushiaji maroketi, uundaji satalaiti, kituo cha kupokea na kuongozea satalaiti na kituo cha kukusanyia data na taarifa za satalaiti.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa kikosi cha anga za mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameashiria satalaiti ya Nour ambayo imewekwa angani umbali wa kilomita 500 kutoka ardhini na kueleza kwamba, mnamo mwaka huu roketi jipya la kubebea satalaiti la Qaem litarushwa kutumwa anga za mbali.

Kuhusiana na kuongezeka uwezo wa Iran wa kuunda ndege zisizo na rubani yaani droni, Jenerali Hajizadeh amesema, makombora ya kutungulia ndege yakiwa yamebeba droni ni ubunifu ulioanzishwa na Iran na kwamba makombora ya aina hiyo yapo kwa wingi nchini.

Kamanda wa kikosi cha anga za mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia droni ya Gaza, ambayo amesema ni moja ya maelfu ya droni zilizobuniwa na kikosi cha anga za mbali cha IRGC na akabainisha kuwa: maadui, ikiwemo Marekani wanasema, baada ya miaka 80 sekta hii ndogo ya ndege zisizo  na rubani imehitimisha enzi za wao kuwa na uwezo wa juu zaidi katika sekta ya anga.

Jenerali Hajizadeh ameongezea kwa kusema, inapasa kulitafakari kwa kina suala hili inapofikia hatua ya adui mwenyewe kukubali na kukiri juu ya uwezo huo wa Iran.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *