Wizara ya mambo ya nje ya Iraq imeonyesha msimamo wake wa kwanza kuhusiana na taarifa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kutangaza kuwa, matini ya taarifa hiyo inaunga mkono misimamo ya nchi hiyo.
Jumatano iliyopita, Uturuki ilishambulia mji wa kitalii wa Zakho ulioko kwenye mkoa wa Dahok nchini Iraq na kuua watu wasiopungua tisa wakiwemo watoto wadogo na kuwajeruhi wengine 23.
Kufuatia hujuma hiyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa taarifa, ambayo bila kutaja jina la Uturuki, imelaani shambulio la mkoani Dahok katika eneo la Kurdistan ya Iraq na kutangaza uungaji mkono wake kwa umoja wa ardhi yote, mamlaka na kujitawala kwa nchi ya Iraq.
Katika taarifa yake hiyo, Baraza la Usalama la UN limezitaka nchi zote wanachama kuunga mkono na kutoa mashirikiano kamili kwa serikali ya Iraq na maafisa wengine husika katika uchunguzi unaofanywa juu ya shambulio hilo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iraq Ahmad As-Sahaaf ameeleza kwamba taarifa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kulaani hujuma dhidi ya mamlaka ya utawala ya Iraq ni ya kwanza ya aina yake kuhusiana na ukiukaji mamlaka ya kujitawala na usalama wa nchi hiyo unaofanywa na Uturuki.
Waziri wa mambo ya nje wa Iraq Fuad Hussein amelizungumzia shambulio la siku ya Jumatano iliyopita lililofanywa na Uturuki katika mji wa kitalii wa Zakho akisema, tangu mwaka 2018 hadi sasa, Ankara imekiuka mamlaka ya kujitawala ya Iraq zaidi ya mara 22,700; na wizara ya mambo ya nje ya Iraq imetoa hati 296 za kulalamikia mashambulio na uchokozi unaofanywa na Uturuki dhidi ya nchi hiyo.