Nukta nne za kistratijia katika matamshi ya Sayyid Nasrullah kwa mnasaba wa kuadhimisha miaka 40 ya Hizbullah

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah, juzi usiku (tarehe 25 Julai) alizungumza na televisheni ya al-Mayadeen kwa mnasaba wa mwaka wa 40 wa kuasisiwa Hizbullah, ambapo nukta kadhaa za kistratijia zilijadiliwa.

Jambo la kwanza lilikuwa kwamba Hiizbullah ya Lebanon imejiimarisha katika mlingano wa nguvu. Uwezo huo ni mkubwa kiasi kwamba adui Mzayuni anafahamu vyema nguvu ya kijeshi na azma imara ya Hizbullah ya kujitetea, na jambo hilo pia liliufahamisha utawala wa Kizayuni kwamba, nguvu ya Muqawama ni kubwa zaidi kuliko suala la mzozo wa mpakani, na kwamba hatua yoyote ile ya kichokozi itakabiliwa na mfano wake. Kwa msingi huo, hii leo adui Mzayuni hathubutu kuchukua hatua yoyote dhidi ya Lebanon. Zaidi ni kwamba, Sayyid Hassan Nasrullah amesema: “Hizbullah ina ndege zisizo na rubani ambazo zimeingia katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina (Israel) mara makumi kadhaa, lakini Israel haikuziona ndege hizo.”

Jambo la pili la kimkakati ni kwamba siasa za kijiografia (jiopolitiki) za Mashariki ya Kati ndio muhimu zaidi kwa Marekani na sio watawala wa nchi za eneo hilo. Rais wa Marekani, Joe Biden hivi majuzi alitembelea Saudi Arabia licha ya kwamba hapo awali alikuwa akiikosoa vikali Riyadh hasa Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo, na alisema waziwazi kuwa ataitenga Saudi Arabia katika jamii ya kimataifa. Sababu ya safari ya Biden huko Saudi Arabia sio kuonesha upendo na urafiki kwa mamlaka ya Saudia, bali kwa sababu ya haja ya Marekani kwa mafuta ya nchi hiyo, haja ambayo imeongezeka zaidi baada ya vita vya Russia dhidi ya Ukraine. Kwa sababu hiyo Sayyid Hassan Nasrullah amesema: “Biden alitembelea eneo la Magharibi mwa Asia kutafuta mafuta.”

Nukta ya tatu ya kistratijia ilikuwa kwamba, tofauti na hitilafu za ndani ya Lebanon ni tishio kubwa kwa nchi hiyo. Hitilafu za kisiasa nchini Lebanon zimesababisha kuendelea kwa hali tete ya kisiasa nchini humo. Utawala wa Kizayuni wa Israel unakaribisha hali hii ya hitilafu na migawanyiko nchini Lebanon kwa sababu unaweza kutekeleza malengo yake ya kijiopoliki, haswa katika maeneo yanayozozaniwa ya nishati katika kivuli cha hitilafu hizo. Akikosoa hali hiyo, Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema: “Serikali ya Lebanon haina uwezo wa kuchukua uamuzi mwafaka wa kulinda rasilimali za nchi. Hivyo, Hizbullah inapaswa kufanya maamuzi kwa lengo la kutetea maslahi na rasilimali za Lebanon.” Matamshi haya ya Sayyid Hassan Nasrullah yalikuwa yakiashiria hatua ya harakati hiyo ya kutuma ndege zisizo na rubani katika medani ya gesi ya Karish siku chache zilizopita.

Nukta ya nne ya kistratijia katika matamshi ya Sayyid Hassan Nasrullah ni kwamba umoja baina ya pande zote za mhimili wa Muqawama ni jambo la lazima na ni nguzo ya kuimarisha nafasi yake. Kuhusiana na hilo, ameashiria vita vya siku 12 vya mwaka jana, ambapo kulikuwa na mshikamano kati ya wanamuqawama katika kuihami Palestina. Katika mkondo huo, Sayyid Hassan Nasrullah ameashiria mzozo kati ya Hamas na Syria katika muongo uliopita na kusema: “Hakuna utawala wowote wa Kiarabu ulioisaidia Hamas kama Syria. Ndugu zetu wa Hamas wamefikia hitimisho kwamba hawawezi kuipa mgongo Syria kwa sababu nchi hiyo ni sehemu ya mhimili wa Muqawama.”

Matamshi haya ya Sayyid Hassan Nasrullah yanasisitiza ukweli kwamba ni lazima kwa wachezaji wakuu wa kambi ya Muqawama na mapambano kuweka kando baadhi ya hitilafu zao na kudumisha mshikamano na umoja wao ili kukabiliana na maadui wao wa pamoja. Hapana shaka yoyote kwamba, umoja wa wanamuqawama ndio sababu kuu ya kufeli siasa za wapinzani wao hususan Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *