Iran inaunga mkono kikamilifu sera ya ‘China Moja’, inapinga ‘uharibifu’ wa Marekani

Rais wa Iran Ebrahim Raisi anasema kuheshimiwa mamlaka ya kitaifa na kulindwa mipaka ya ardhi ya nchi ni miongoni mwa kanuni za kimsingi za sera za kigeni za Tehran huku akitangaza uungaji mkono thabiti wa Jamhuri ya Kiislamu kwa sera ya China Moja kuhusiana na Taiwan.

Uungaji mkono kwa sera ya China Moja ni sera ya uhakika na ya msingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran,” Raisi amesema katika mazungumzo ya simu ya saa moja na Rais wa China Xi Jinping siku ya Ijumaa.

Amesema uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi zingine ni mwendelezo wa siasa haribifu za Washington za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja, ambazo sasa “zinageuka kuwa tishio kwa amani na usalama wa kimataifa.”

Pia katika mazungumzo ya simu ya Ijumaa, Raisi alimwambia mwenzake wa China kwamba Tehran imeazimia kupanua uhusiano na Beijing katika nyanja zote bila kujali matukio ya kimataifa yaliyopo na akasema juhudi zozote za Marekani za kurudia zama za Vita Baridi duniani zitaashiria udhaifu na kupungua satwa yake.

Akiashiria mazungumzo kati ya Iran na kundi la 4+1 kuhusu njia zinazowezekana za kufufua mapatano ya nyuklia ya 2015, yanayojulikana rasmi kwa jina la Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), Raisi amesema kama mhusika aliyekiuka makubaliano hayo, Marekani inapaswa kuchukua “uamuzi wa kisiasa” na kuchukua hatua zote muhimu za kuondoa vikwazo haramu dhidi ya Tehran na pande za tatu.

Kwa upande wake, Rais Xi wa China amesema Iran ina mchango mkubwa katika kudumisha uthabiti katika eneo hili na kuashiria upinzani wa nchi yake dhidi ya sera ya mashinikizo na kuegemea upande mmoja.

Amesema kutokana na hali tata ya kimataifa, China na Iran zimeimarisha mshikamano, ushirikiano, maslahi yao ya pamoja na kulinda haki na maslahi halali ya nchi zinazoendelea.

Amesisitiza umuhimu wa uhusiano wa kimkakati kati ya Tehran na Beijing na kusema China iko tayari kufanya kazi na Iran ili kusukuma maendeleo mapya ya ushirikiano wa kimkakati wa kina kati ya nchi hizo mbili.

Rais wa China amezitaka nchi hizo mbili ziendelee kuunga mkono kithabiti masuala yanayohusu maslahi yao ya msingi huku akiongeza kuwa Tehran na Beijing zinahitaji kudumisha mawasiliano ya karibu kuhusu utekelezaji wa mipango yao ya ushirikiano wa kina.

Raisi na Xi pia wamepongeza ongezeko la mabadilishano ya kibiashara baina ya nchi mbili katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na wameafikiana kuhusu njia za kuharakisha utekelezaji wa mapatano ya kistratijia ya miaka 25 yaliyofikiwa baina ya China na Iran.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *