Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov ameionya vikali Marekani na nchi wanachama wa muungano wa kijeshi wa NATO kuhusu kuendelea kuipa Ukraine silaha na kusema hatua hiyo itarefusha vita na kuzidisha machungu.
Lavrov aliyasema hayo Ijumaa katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, katika mazungumzo yao ya kwanza ya simu tokea Russia ianzishe oparesheni ya kijeshi nchini Ukraine mnamo Februari 24.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Lavrov amesema: “Hatua ya Marekani na NATO ya kuendelea kulimiminia jeshi la Ukraine silaha itarefusha vita na masaibu ya utawala wa Kiev sambamba na kuongeza idadi ya wanaofariki dunia.” Hadi sasa utawala wa Rais Biden wa Marekeni umeipa Ukraine silaha zenye thamani ya dola bilioni 7.6.
Lavrov amesema Russia inakaribia kufikia malengo yake katika oparesheni yake ya kijeshi Ukraine ambayo ilianzishwa kwa lengo la kujihami. Russia inasisitiza kuwa oparesheni yake hiyo inalenga kuondoa hali ya kijeshi katika eneo la mashariki mwa Ukraine la Donbas.
Mwaka 2014 majimbo ya Donetsk na Luhansk, ambayo kwa pamoja yanaunda eneo la Donbas, yalijitangaza kuwa ni jamhuri huru na yalikataa kuitambua serikali ya Ukraine inayounga mkono na madola ya Magharibi. Tangazo hilo la uhuru lilipelekea kuibuka makabiliano ya kijeshi baina ya jamhuri hizo na jeshi la Ukraine.
Russia imezitambua ramsi jamhuri hizo za Donbass kama nchi huru na imeitaka Ukraine ijitangaze rasmi kuwa nchi isiyoegemea upande wowote ambayo haitajiunga na kambi yoyote ya kijeshi ya Magharibi.
Wakati wa kuamuru oparesheni ya kijeshi Ukraine, Rais Vladimir Putin wa Russia alisema lengo la oparesheni hiyo lilikuwa ni kuwalinda watu ambao kwa miaka minane walikiwa wanakandamizwa na kuuawa kwa umati na utawala wa Kiev.