Wananchi walia na wodi ya wazazi Kibaha

Kibaha. Wananchi wa kata ya Mbwawa mjini Kibaha mkoani Pwani wameiomba Serikali kujengea wodi ya wazazi katika zahanati iliyopo katika kata hiyo ili kusaidia kina mama wajawazito.

Wamesema kuwa kwa sasa wajawazito wanatembea zaidi ya kilometa 10 kwenda katika kata ya Mlandizi kutokana na zahanati hiyo kuosa wodi ya wazazi hali inayohatarisha maisha yao.

Wametoa kero hiyo leo Jumapili Julai 31, 2022 kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubaka Kunenge alipofanya ziara ya kukagua miradi na kusikiliza kero za wananchi huku wakisisitiza kuwa wapo tayari kutoa michango ya hali na mali katika ujenzi wa wodi ya wazazi katika eneo hilo.

Wamesema kuwa ukosefu wa wodi ya wazazi unasababisha baadhi ya wajawazito kujifungulia njiani wakati wa kwenda kwenye zahanati ya jirani.

“Mkuu wa mkoa tunaomba ukafanyie kazi kero zetu, zipo nyingi lakini adhabu kubwa tuliyonayo ni hatuna wodi ya wazazi, tunataka sisi akina mama tujifungulie hapahapa, sio huko Mlandizi ni mbali, unakuta wakati mwingine kutokana na umbali mama anazidiwa njiani anajifungua mwenyewe, ” amesema Asha Matambo

Kwa upande wake Fatuma Kondo amesema kwa sasa wanaomba wodi ijengwe katika zahanati hiyo wakati wakisubiri ujenzi wa kituo cha afya.

Naye dereva wa bodaboda katika eneo hilo amesema “Mimi ni bodoboda napenda niungane na mama zetu kweli wodi ya wazazi tunahitaji hapa, unakuta unambeba mjamzito kumpeleka Mlandizi bahati mbaya kwa umbali mafuta yanaisha au hata kutokea dhoruba yeyote na katikati ya njia kuna msitu mkubwa watakimbia wapi na hakuna nyumba jirani hadi ufike eneo la Vikuruti au Kibwende ” amesema Shomari Kondo

Akijibu changamoto hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ameagiza kuanza ujenzi wa wodi ya wazazi katika zahanati ya Kata ya Mbwawa na kutaka zitumike Sh9 milioni fedha zilizotokana na mauzo ya trekta ya mtaa huo katika kuanza ujenzi wa wodi hiyo

“Kituo cha Afya kitachukua muda kujengwa, Zahanati hii ifanyiwe maboresho kwa kujengwa wodi ya wazazi” ameeleza Kunenge.

Pia Kunenge amewaelekeza wananchi kwa kushirikina na Serikali ya Wilaya kutafuta eneo kubwa la ujenzi wa kituo cha Afya.

“Tutafute eneo muafaka eneo ambalo wananchi watafika kwa urahisi kwa ajili sasa ya ujenzi wa kituo cha Afya ambacho tayari Serikali imetutengea Sh2 bilioni kwa ajili ya ujenzi na vifaa tiba” amesema

 

 

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *