Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndio moyo wa Uislamu na mrengo wa muqawama wa Kiislamu duniani.
Sayyid Hassan Nasrullah alisema hayo jana Jumanne mjini Beirut akiuhutubia umati wa waombolezaji wa Ashura ya Imam Hussein (AS) na kuongeza kuwa, Iran chini ya uongozi wa Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu itaendelea kubeba bendera ya dini tukufu ya Kiislamu na kambi ya muqawama.
Ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu kama roho ya kambi ya muqawama, imeufanyia mengi kwa maneno na vitendo mrengo huo wa mapambano ya Kiislamu.
Sayyid Nasrullah amebainisha kuwa, hii leo (Iran) imeendelea kuonesha uaminifu na mahaba kama ilivyofanya katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, licha ya hali ngumu ya kiuchumi iliyosababishwa na vikwazo na mashinikizo ya maadui.
Kadhalika Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ametoa mkono wa pole kwa Waislamu wa Nigeria, baada ya askari wa serikali ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi kushambulia kumbukumbu za maombolezo ya Ashura ya Imam Hussein AS katika mji wa Zaria na kuua shahidi na kujeruhi kadhaa miongoni mwao.
Aidha Sayyid Hassan Nasrullah ameashiria ukatili wa vikosi vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Gaza na kubainisha kuwa, “Tunawapongeza wanajihadi wa kambi ya muqawama ya Palestina na mashahidi waliojitoa muhanga wakijibu mapigo ya uchokozi wa Wazayuni. Lakini msimamo wa wale wanaodai kuwa Waislamu kwa damu za Wapalestina waliouawa shahidi ni upi?”
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameongeza kwa kusema, harakati hiyo itaendelea kusimama mstari wa mbele dhidi ya adui Mzayuni, huku akiuonya utawala huo haramu kwamba utakabiliwa kwa mapigo makali iwapo utathubutu kuivamia ardhi ya Lebanon.