FARAAN: Siku ya kuapishwa kwa Rais wa Tano wa Kenya itakuwa sikukuu ya kitaifa, kamati ya kusimamia kuhamishwa kwa mamlaka kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta hadi kwa mrithi wake ilisema Ijumaa.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua, ilifanya kikao chake cha kwanza.
Bw Kinyua alisema kamati hiyo inangojea Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutangaza mshindi wa urais ili kuanza shughuli zake kikamilifu.
Bw Kinyua alisema kamati hiyo iko tayari kuanza majukumu yake ambayo yanajumuisha kutoa ulinzi kwa rais mteule.
Kamati hiyo itahakikisha kuwa rais mteule anakutana na wakuu wa idara mbalimbali za serikali ili kumpa taarifa.
Kamati hiyo inajumuisha Bw Kinyua, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i, Katibu wake Karanja Kibicho, Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai, Jenerali Robert Kibochi, Mkuu wa Idara ya Ujasusi (NIS) Philip Kameru, Msajili wa Mahakama Anne Amadi, Kinuthia Mbugua, Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki na Makatibu wa Wizara Jerome Ochieng, Julius Muia, Macharia Kamau, Julius Korir, Joe Okudo na Wakili Mkuu wa Serikali Ken Ogeto.
“Tutaanza rasmi maandalizi baada ya IEBC kutangaza mshindi wa urais wa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9,” akasema Bw Kinyua.
Kamati hiyo pia imetwikwa majukumu ya kuwezesha mawasiliano kati ya Rais Kenyatta na rais mteule.