Wanachama 13 wa genge la kigaidi la al Shabab waangamizwa Somalia

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, wanachama 13 wa genge la kigaidi ukufurishaji la al Shabab wameangamizwa katika shambulio la anga lililofanywa katikati ya Somalia.

Maafisa wa kijeshi wa Somalia wametangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, shambulio la anga lililofanywa nchini humo dhidi ya maficho ya magaidi wa al Shabab katika mkoa wa Hiran limeua wanamgambo wasiopungua 13.

Shambulio hilo limefanyika kwa kushirikishwa jeshi la Somalia na ni la pili kufanywa dhidi ya magaidi wa al Shabab katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

Tangu mwaka 1992, Somalia haijawahi kuwa na utulivu wa japo siku moja kutokana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na mashambulizi ya genge la kigaidi la al Shabab.

Genge hilo lilianzishwa mwaka 2004 na lenyewe limejitangaza kuwa ni sehemu ya mtandao wa kigaidi wa al Qaida.

Huko nyuma pia kikosi cha AU kilitangaza kwamba kimefanya mashambulizi matatu ya anga dhidi ya genge la al Shabab katika mkoa wa Hiran.

Genge hilo mara kwa mara limekuwa likishambulia wanajeshi wa serikali na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika hasa katika mji mkuu Mogadishu na pia huwa linafanya mashambulizi ya mara kwa mara ya raia wa Somalia.

Kikosi cha kulida amani cha Umoja wa Afrika kiko nchini Somalia kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa. Kikosi hicho kina karibu askari 20,000 ambao ni kutoka Uganda, Ethiopia, Burundi na Kenya.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *