Khatibu wa Msikiti wa al Aqsa katika mji mtakatifu wa Quds huko Palestina amesema kuwa, Msikiti huo mtakatifu bado uko kwenye moto wa jinai za Wazayuni lakini wananchi wa Palestina wataendelea kuwa mstari wa mbele kuulinda.
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ya Palestina OIC imeitangaza tarehe 21 Agosti kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Misikiti ili kuibakisha hai siku ambayo Wazayuni waliuchoma moto Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu. Jinai hiyo ilifanywa na Wazayuni tarehe 21 Agosti, 1969.
Kwa mnasaba huo, leo Jumapili Dk. Yusuf Juma Salama, waziri wa zamani wa wakfu na masuala ya kidini wa Palestina amefanyiwa mahojiano na shirika la habari la Iran Press katika mji mtakatifu wa Baytul Muqaddas na kusema kuwa, viongozi wa utawala wa Kizayuni wanaonesha waziwazi chuki zao dhidi ya Msikiti wa al Aqsa kwa kujaribu kuugawa Msikiti huo kieneo ni kiwakati ili kuruhusu wasio Waislamu waingie bila ya heshima Msikitini humo, lakini Wapalestina wataendelea kusimama imara kuulinda.
Sheikh Yusuf Juma Salama amesisitiza pia kuwa, Msikiti wa al Aqsa ni eneo takatifu la Waislamu na kwamba yeyote asiye Muislamu hana haki yoyote ndani Msikiti huo. Pia amesema, jukumu la kukilinda Kibla hicho cha Kwanza cha Waislamu ni la kila Muislamu popote pale alipo duniani, si la Wapalestina peke yao.
Hata Umoja wa Mataifa nao ulitoa aziio nambari 271 la mwaka 1969 la kulaani jinai ya Israel ya kuuchoma moto Msikiti wa al Aqsa.