Jumapili ya jana tarehe 21 Agosti ilisadifiana na kutimia mwaka wa 53 tangu kuchomwa moto Msikiti mtakatifu wa al-Aqswa, kibla cha kwanza cha Wiaslamu, jinai ambayo ilifanywa na utawala vamizi wa Israel ambapo walimwengu walibakia kuwa watazamaji tu na kutoonyesha radiamali yoyote kwa kitendo hicho cha kinyama.
Tarehe 21 Agosti 1969 Mzayuni mmoja aliuchoma moto msikiti huo ukiwa ni uthibitisho mwingine wa jinai kubwa za utawala wa Kizayuni.
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ya Palestina OIC imeitangaza tarehe 21 Agosti kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Misikiti ili kuibakisha hai siku ambayo Wazayuni waliuchoma moto Msikiti wa al Aqswa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu.
Tukio la kuuchomwa moto Msikiti wa al-Aqswa liliamsha hasira na ghadhabu za Waislamu duniani kote. Aidha utawala wa Kizayuni uliilinasibisha tukio hilo na mtalii mmoja Myahudi mwenye misimamo ya kufurutu ada raia wa Australia aliyejulikana kwa jina la Denis Michael. Mtalii huyo alifikishwa mahakamani na kuhukumiwa kimaonyesho tu na kisha akaachiwa huru kwa madai kwamba eti alikuwa mgonjwa wa akili.
Katika tukio la kuchomwa moto Msikiti wa al-Aqswa kwa akali mita mraba 200 za eneo la juu la msikiti huo liliharibika kabisa, sehemu tano za mnara wa msikiti huo ziliungua. Hatua hiyo ililaaniwa vikali na akthari ya mataifa, lakini kivitendo hakuna nchi ambayo ilijitokeza na kutangaza himaya na uungaji mkono wake kwa matukufu ya Kiislamu ya Palestina.
Hivi sasa licha ya kupita zaidi ya miongo mitano tangu kutokea tukio hilo, wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel wameuzingira msikiti huo na wamechimba njia nyingi za chini kwa chini kuelekea katika msikiti huo lengo likiwa ni kuandaa uwanja na mazingira ya kubadilisha utambulisho wa Kiislamu wa msikiti huo.
Dawood Shahab, mjumbe mwandamizi wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina alisema Jumapili ya jana katika mazungumzo yake na Shirika la Habari la Iran Press kwamba, moto huo unakumbusha masuulia na majukumu ya Waislamu kwa ajili ya kuulinda na kuuhami Msikiti wa al-Aqswa. Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Jihadul Islami aliongeza kusema kuwa, mtoto katika msikiti bado haujazimika; kwani hujuma, mashambulio na uchimbaji wa mashimo kuelekea katika msikiti huo vingali vinaendelea.
Sheikh Ikrima Sabri Khatibu wa msikiti mtakatifu wa al-Aqswa, akizungumza kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mwaka ambao Wazayuni walikichoma moto Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa al Aqsa huko Palestina amesema kuwa, moto dhidi ya msikiti huo ungali unawaka kupitia vitendo kama vya kuuvamia msikiti huo mara kwa mara uvamizi ambao unafanywa na walowezi wa vitongoji vya Kizayuni.
Kadhalika amesema, kuporwa ardhi za Wapalestina, kuyayahudisha maeneo ya Wapalestina, kamatakamata ya kiholela na kuwalazimisha Wapalestina kuwa wakimbizi na hatua mbalimbali za kibaguzi zinazofanywa na viongozi wa utawala ghasibu yote hayo ni mifano ya wazi kabisa inayoonyesha kuwa, moto dhidi ya msikiti wa al-Aqswa ungali unawaka na haujazimika.
Kwa upande wake, Nasser Kan’ani Chafi msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akizungumzia tukio la kuchomwa moto msikiti wa al-Aqswa miaka 53 iliyopita amesema, Misikiti yote duniani itaendelea kuwa vituo vya muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni hadi zitakapokombolewa ardhi zote za Palestina. Aidha amesema, mapambano na muqawama ndiyo njia pekee ya kuiokoa Palestina na Msikiti wa al-Aqswa na kwamba Misikiti yote duniani itaendelea kuwa vituo vya mapambano na muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel hadi ardhi zote za Palestina zitakapokombolewa kikamilifu.
Kwa upande wake, Dkt. Yusuf Juma Salama, waziri wa zamani wa wakfu na masuala ya kidini wa Palestina amesema, viongozi wa utawala wa Kizayuni wanaonesha waziwazi chuki zao dhidi ya Msikiti wa al Aqsa kwa kujaribu kuugawa Msikiti huo kieneo ni kiwakati ili kuruhusu wasio Waislamu waingie bila ya heshima Msikitini humo, lakini Wapalestina wataendelea kusimama imara kuulinda.
Kadhalika Sheikh Yusuf Juma Salama amesisitiza kuwa, Msikiti wa al Aqsa ni eneo takatifu la Waislamu na kwamba yeyote asiye Mwislamu hana haki yoyote ndani Msikiti huo na kwamba, jukumu la kukilinda Kibla hicho cha Kwanza cha Waislamu ni la kila Mwislamu popote pale alipo duniani, na si la Wapalestina peke yao.
Imepita zaidi ya nusu karne tangu Msikiti huo uchomwe moto. Hii leo Msikiti wa al-Aqswa unakabiliwa na njama za kila namna ambazo ni chuki na uadui wa Wazayuni ambao lengo lake ni kubadilisha utambulisho wa msikiti huo na kuupa sura ya Uyahudi.
Hii ni katika hali ambayo, viongozi na watawala wa mataifa ya Kiarabu wameendelea kutanguliza mbele maslahi yao binafsi na ya kikaumu mbele ya maslahi ya ulimwengu wa Kiislamu. Baya zaidi ni hatua ya baadhi ya madola ya Kiarabu ya kulisaliti taifa la Palestina na malengo yake baada ya kuamua kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel ambao unatenda jinai kila uchao dhidi ya Wapalestina.
Hapana shaka kuwa, siasa za namna hii zinazotekelezwa na viongozi wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu zimewafanya Wazayuni washadidishe njama zao dhidi ya Msikiti wa al-Aqswa na Beitul-Muqaddas bila ya wasiwasi wowote.