Afisa mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuunga mkono harakati za ukombozi wa Palestina.
Mahmoud al-Zahar ameyasema hayo Jumatatu katika mahojiano na Radio ya Al Aqsa. Amesema Iran imekuwa ikiunga mkono harakati dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unakalia kwa mabavu ardhi za Palestina.
Ameongeza kuwa: “Tunaishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuunga mkono Mhimili wa Muqawama na sasa tuko katika ukingo wa mapamabano ya Ahadi ya Mwisho, na hivyo lazima tujitayarishe kwa ajili ya mapambano hayo.”
Afisa hiyo wa Hamas amesema uhusiano wa harakati hiyo na nchi zingine za Kiarabu na Kiislamu pamoja na nchi zingine zote duniani uko katika msingi wa ukombozi wa Palestina. Akiashiria uhusiano wa Hamas na Misri amesema uhusiano huo ni muhimu kwani Cairo ina nafasi muhimu katika kadhia ya Palestina.
Al Zahar pia amegusia mapambano ya harakati za Palestina katika Ukingo wa Magharibi na kusema: “Harakati za muqawama na mapambano katika Ukingo wa Magharibi zimepelekea utawala wa Kizayuni wa Israel uingiwe na kiwewe na uchanganyikiwe kwani hali katika eneo hilo ni sawa na ya mapambano ya Ukanda wa Gaza.” Amesema hivi sasa kunashuhudiwa Wapalestina wakiuawa shahidi katika Ukingo wa Magharibi na hilo linaashiria kushika kasi mapambano.