Kundi la raia wa Kenya limeifungulia mashitaka serikali ya Uingereza katika Mahakama ya Haki za Binadamu ya Ulaya, likitaka iwajibishwe kwa jinai ilizotenda dhidi ya wananchi wa Kenya enzi za ukoloni.
Katika faili hilo, Wakenya hao wamesema mababu zao waliteswa na kukandamizwa na wakoloni Waingereza, mbali na kufukuzwa kwenye ardhi zao.
Wakili Joel Kimutai Bosek anayeliwakilisha kundi hilo la raia wa Kenya amesema jinai hizo zilifanywa na wakoloni wa Uingereza katika eneo la Kericho, magharibi mwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki. Eneo hilo ni maarufu kwa kilimo cha majani chai, moja ya bidhaa ambazo Kenya inauza kwa wingi nje ya nchi.
Bosek amesema serikali ya London imekuwa ikikwepa kusikiliza shauri lao hilo, na kwa msingi huo wamelazimika kuwasilisha malalamishi yao kwa Mahakama ya Haki za Binadamu ya Ulaya.
Wakenya hao wanataka kulipwa fidia kwa jinai walizotendewa mababu zao enzi za ukoloni, mbali na kupokonywa ardhi zao, haswa zilizokuwa na rotuba kwa ajili ya uzalishaji wa majani chai.
Itakumbukwa kuwa, Oktoba mwaka 2019, Wakenya 100,000 waliwasilisha mashtaka kwa Umoja wa Mataifa dhidi ya utawala wa kikoloni wa Uingereza kutokana na jinai ya kuwapora ardhi zao zenye rotuba na kuwapeleka sehemu kame.
Mwaka 2013, serikali ya Uingereza ililazimika kuomba radhi na kukubali kuwalipa fidia maelfu ya wapiganaji wa vita vya uhuru wa Kenya vilivyojulikana kama Mau Mau, kutokana na kuteswa na kutendewa maovu katika miaka ya 1950. Tume ya Haki za binadamu ya Kenya inakadiria kwamba Wakenya 90,000 waliuliwa au kukatwa viungo vyao na karibu 160,000 kufungwa, na wengine wengi kuteswa na kubakwa katika zama za ukoloni wa Uingereza