Edward “Ned” Price, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani alisema jana Jumatano kuwa, Washington imetoa majibu kuhusu mitazamo ya Iran juu ya mazungumzo ya kuondolewa vikwazo Tehran. Amesema: Uchunguzi wetu kuhusu mitazamo ya Iran umekamilika na leo (Jumatano) tumekabidhi mapendekezo yetu kwa Umoja wa Ulaya.
Naye Nasser Kan’ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, Tehran imepokea majibu ya Marekani kuhusu kutatuliwa masuala yaliyobakia katika mazungumzo ya kuondolewa vikwazo Iran. Amesema majibu hayo imepatiwa Iran kupitia mratibu wa Ulaya wa mazungumzo hayo Jumatano jioni. Pia amesema, uchunguzi wa kina kuhusu mitazamo hiyo ya Marekani umeanza na baada ya kukamilisha uchunguzi wake, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatoa maoni yake na kuyakabidhi kwa mratibu wa mazungumzo hayo.
Majibu ya Marekani yametolewa katika hali ambayo viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo wanaendelea kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran. Msemaji wa Ikulu ya Marekani (White house), Karine Jean-Pierre amesema mapema leo Alkhamisi kuwa, rais wa nchi hiyo Joe Biden amekusudia kikweli kweli kuizuia Iran kupata kile alichodai silaha za nyuklia. Karine Jean-Pierre amerejea madai ya kila siku ya nchi yake akisema, njia bora kabisa kwetu sisi (Marekani) kuhusu Iran ni kutumia njia za kidiplomasia na tunasubiri kuona je tutaweza kufikia makubaliano?
Kabla ya hapo pia, John Kibry, mratibu wa mawasiliano ya kiistratijia wa baraza la usalama wa taifa la White House naye alikiri kuwa kitendo cha rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump cha kujitoa kiholela katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA mwaka 2018, yamepelekea kutengwa Marekani. Lakini wakati huo huo aliituhumu Iran kuwa haikuheshimu kikamilifu makubaliano hayo. Alidai pia kuwa Marekani ina nia ya kweli ya kufufua mapatano hayo ya kimataifa. John Kirby aliendeleza pia madai kuhusu mradi wa nyuklia wa Iran kwa kusema, Marekani imetangaza waziwazi na kuwaeleza Wairani kupitia njia maalumu kwamba inapaswa kujibu maswali ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA. Amedai, hiyo ndiyo njia pekee ya kuweza kuondowa wasiwasi uliopo.
Tuhuma hizo za viongozi wa Marekani zinatolewa katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mara zote imekuwa ikitangaza kuwa, si tu mradi wake si wa kutengeneza silaha za nyuklia lakini hata hauelekei kabisa upande huo wa kutengeneza silaha hizo za maangamizi ya umati. Kutokana na itikadi na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu, ni haramu kumiliki silaha za maangamizi ya umati, ziwe za nyuklia au zozote zile. Dunia nzima pia inatambua kuwa, mradi wa nyuklia wa Iran ni wa amani kikamilifu na hata mashirika ya kimataifa kama IAEA yamethibitisha mara chungu nzima kuwa, mradi wa nguvu za nyuklia wa Iran ni wa kiraia na ni wa amani kikamilifu. Sasa kujitokeza viongozi wa Marekani na kukanusha uhakika huo wote na badala yake kuanza kutoa tuhuma zisizo na mashiko, hakutokani na jambo lolote ila kuendeleza tu siasa za kibeberu za dola hilo la kiistikbari na kurejea madai yake yale yale ya uongo ya kila siku.
Wakati huo huo na sambamba na kuenea baadhi ya habari kuhusu yaliyomo kwenye majibu ya Marekani kuhusu mapendekezo ya Iran, tayari kumeenea uvumi kwamba Washington imeendelea kama kawaida yake, kukwamisha mazungumzo hayo. Baada ya kutangaza kutangaza kutolewa majibu ya Marekani kwa mapendekezo ya Iran, Ned Price msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani amesema pia kuwa, bado kuna maudhui kubwa hazijapatiwa ufumbuzi. “Kuna baadhi ya mipasuko ambayo nayo inabidi izibwe,” amedai.
Kwa upande wake, Mikhail Ivanovich Ulyanov, mwakilishi wa Russia katika mazungumzo ya Vienna amejibu matamshi hayo ya msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani na kusema, Wamarekani wana sifa moja ya ajabu sana nayo ni kwamba kila pale wanapoona tumekaribia mwishoni kabisa mwa mazungumzo, wanazusha matatizo mapya.
Tukiachana na maelezo yoyote yaliyomo kwenye majibu ya Marekani, msimamo wa Iran utaendelea daima kuwa ni ule ule wa kutokubali kabisa kuvukwa mistari yake myekundu na mpaka kwanza ijikinaishe kuwa ni kweli vikwazo dhidi yake vimeondolewa, ndipo hapo itakapoamini kwamba mapatano ya JCPOA yamefufuliwa.