Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesisitiza kuwa, kujeruhiwa askari wa utawala dhalimu wa Israel katika mapigano katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni ishara ya wazi ya sisitizo la vijana wa Kipalestina juu ya kupambana na uvamizi wa utawala ghasibu wa Israel
Hazim Qassim amebainisha kuwa, vita na utawala vamizi wa Quds viko wazi katika maeneo yote ya Palestina na tena ni vya pande zote na kwamba, dhulma na jinai za utawala haramu wa Israel haviwezi kutia dosari azma ya wananchi wa Palestina katika harakati yao ya muqawama na mapambano.
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ameongeza kuwa, Wapalestina hawawezi kuacha muqawama na mapambano kwani hilo ndilo chaguo lao pekee la kuzikomboa ardhi zao kutoka katika makucha ya adui Mzayuni.
Kiongozi huyo wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ameongeza kuwa, jinai za wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan katu haziwezi kuzuia wimbi la muqawama na mapambano katika eneo hilo.
Tathhmini mbalimbali zinaonyesha kuwa, muqawama uko chini ya mwavuli wa uungaji mkono wa kivitendo wa Wapalestina na jambo hilo ndilo linalozidi kutia nguvu harakati za muqawama katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, viongozi mbalimbali wa harakati za mapambano huko Palestina wameendelea kusisitiza kwamba, hakuna chaguo jingine la kuzikomboa ardhi za Palestina ghairi ya muqawama na mapambano dhidi ya Wazayuni maghasibu.