Azimio la Ukraine dhidi ya Russia katika Umoja wa Mataifa lapingwa na nchi nyingi

Rasimu ya azimio la Ukraine la kutaka Russia ilaaniwe katika Umoja wa Mataifa limegonga mwamba baada ya kupingwa na aghalabu ya nchi za dunia.

Azimio hilo limeungwa mkono na nchi 58 pekee kati ya nchi zote 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa ikiwa ni idadi ndogo sana ikilianganishwa na nchi ambazo ziliunga mkono Kiev mwezi Machi katika Baraza la Usalama. Katika kikao cha Machi nchi 141 ziliunga mkono Ukraine lakini mara hii ni asilimia 30 tu ya nchi zilizounga mkono azimio hilo la kuilaani Russia. Nchi zote za Afrika na Ghuba ya Uajemi hazikuunga mkono azimio hilo dhidi ya Russia.

Balozi wa Ukraine katika Umoja wa Mataifa Sergey Kislitsa aliwasilisha azimio hilo Jumatano kwa mnasaba wa siku ya uhuru wa nchi  hiyo. Kikao hicho kilijumuisha hotuba kwa njia ya video ya Rais Vladimir Zelensky wa Ukraine na taarifa kadhaa za nchi za Magharibi ambazo zililaani Russia. Balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia alipinga tuhuma hizo huku akiwasilisha ushahidi wa kutosha kuhusu jinai za Ukraine na hata kuzitaja nchi za Magharibi ambazo ni washirika wa jinai hizo.

Hayo yanajiri huku Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia akisema nchi hiyo haitasitisha operesheni yake maalumu ya kijeshi ndani ya ardhi ya Ukraine mpaka iyafikie malengo yake yote.

Dmitry Medvedev, ambaye pia ni rais wa zamani wa Russia ametangaza kuwa, lazima malengo yote ya operesheni maalumu ya kijeshi ya nchi hiyo ndani ya Ukraine yafikiwe. Tarehe 24 Februari, Rais Vladimir Putin wa Russia alitoa amri ya kuishambulia kijeshi Ukraine ikiwa ni katika kuitikia ombi la viongozi wa maeneo mawili ya Donetsk na Luhansk mashariki ya nchi hiyo, lakini akatangaza kuwa lengo la Moscow ni kuipokonya silaha tu Ukraine na si kuikalia ardhi ya nchi hiyo.

Hii ni katika hali ambayo, nchi za Magharibi na hasa Marekani na Uingereza zimechukua hatua ya kuiwekea Russia vikwazo vya kila aina sambamba na kuipatia Ukraine aina mbali mbali za silaha na zana za kivita ili kuizuia Kyiv isiketi kwenye meza ya mazungumzo ya suluhu na Russia na kushadidisha pia vita na mapigano nchini humo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *