Wizara ya Afya ya Yemen imetangaza takwimu mpya za hasara roho na mali za watu zilizosababishwa na jinai za miaka minane ya vita vya kivamizi vya muungano wa nchi za Kiarabu wakiongozwa na Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati).
Mwaka 2015, Saudia na Imarati kwa baraka kamili za Marekani, nchi za Magharibi na utawala wa Kizayuni wa Israel, zilianzisha vita vya kivamizi na kijinai vya pande zote dhidi ya wananchi Waislamu wa Yemen.
Madola hayo vamizi yametenda jinai kubwa sana katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu kiasi kwamba, kila leo kunatolewa takwimu mpya za jinai hizo za kutisha.
Jana Jumamosi, Agosti 27, 2022, Wizara ya Afya ya Yemen ilitangaza kuwa, hadi hivi sasa, raia 15,483 wa Yemen wamethibitishwa kuuliwa kikatili na muungano vamizi wa Saudi Arabia, 31,598 wamethibitishwa kujeruhiwa huku asilimia 25 ya waliouawa na kujeruhiwa wakiwa ni wanawake na watoto wadogo.
Wavamizi hao wametumia silaha nyingi zilizopigwa marufuku na wamesababisha kuongezeka mno idadi ya mama wanaoharibu mimba zao kutoka 12,000 hadi laki tatu na 50,000 katika kipindi cha baina ya mwaka 2015 hadi 2021.
Wizara ya Afya ya Yemen pia imesema katika ripoti yake ya jana kuwa, kuendelea vikwazo na kuzingirwa kila upande Yemen kumeongeza idadi ya watoto wanaozaliwa na viungo pungufu na idadi hiyo imeongezeka hadi watoto 22,599 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Wayemen waliokumbwa na maradhi ya sarani na magonjwa mengine hatari yakiwemo ya kiakili, imeongezeka kwa asilimia 50 tangu mwaka 2015 vilipoanza vita hivyo vya kivamizi hadi mwaka jana 2021.