Zaidi ya maafisa 8,000 wa polisi wa Somalia wapewa mafunzo na kikosi cha AU

Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia kimetoa mafunzo na ushauri wa kiusalama kwa maafisa polisi 8,167 wa Somalia kikosi hicho kilipotumwa kwa mara ya kwanza nchini humo mwaka 2009.

Mkuu wa Polisi wa Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS), Rex Dundun amesema hayo na kuongeza kuwa, maafisa wa polisi walioajiriwa na waliopewa mafunzo sasa wanasimamia sheria na kuimarisha amani na utulivu katika maeneo yaliyokombolewa kutoka kwa genge la kigaidi na ukufurishaji la al-Shabab nchini humo.

“Tuna muda mfupi tu wa kuliandaa jeshi la polisi la Somalia kushughulikia usalama wake wa ndani. Tunakimbizana na wakati,” amesema Dundun kwenye taarifa iliyotolewa katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu.

Inatarajiwa kuwa Vikosi vya Usalama vya Somalia (SSF) vitachukua majukumu ya kulinda usalama kutoka kwa kikosi hicho cha AU ifikapo mwezi Disemba 2024.

Sehemu kubwa ya maafisa hao wa polisi wa Somalia waliopata mafunzo hayo ni kutoka Jubaland, Hirshabelle na maeneo ya kusini magharibi mwa nchi hiyio ikiwemo pia Mogadishu.

Dundun amesema mafunzo hayo yanahusu masuala kama vile usimamizi, usalama wa uchaguzi, haki za binadamu, kikosi cha usalama wa barabarani, polisi jamii na kuzuia unyanyasaji wa kijinsia.

Afisa huyo wa AU pia amesema, Polisi wa ATMIS wamejenga, kukarabati na kuvipa vifaa takriban vituo 20 vya polisi vya Somalia ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa kuboresha miundombinu ya kiusalama nchini humo.

Somalia inalenga kuajiri idadi ya kutosha ya wafanyakazi wa jeshi la polisi si kwa ajili tu ya kusimamia sheria na kulinda usalama na utulivu lakini pia kwa ajili ya kulisaidia jeshi kukomboa maeneo zaidi kutoka mikononi mwa magaidi wa al Shabab. Mafunzo hayo pia yanalenga kujenga uwezo na kuajiri maofisa vijana wa kuchukua nafasi za wazee.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *