Iran: Utatuzi wa kadhia ya Palestina ni msingi wa utulivu na usalama

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Bagheri Kani amesema utatuzi wa kadhia ya Palestina ndio msingi wa kuanzishwa utulivu na usalama Asia Magharibi (Mashariki ya Kati), na kueleza kwamba mpango wowote unaopuuza haki za taifa la Palestina husababisha kukosekana utulivu na kuvuruga usalama wa eneo hilo.

Bagheri Kani aliyasema hayo katika mkutano wake na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar anayehusika na Masuala ya Kieneo Mohammed bin Abdulaziz al-Khulaifi na ujumbe aliofuatana nao mjini Tehran.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran alilitaja suala la Palestina kuwa ni wajibu wa kibinadamu na Kiislamu kwa nchi zote za eneo, akisisitiza kuwa uthabiti wa eneo unategemea kurejeshwa kikamilifu haki za Wapalestina.

Bagheri Kani aliendelea kuashiria juhudi zinazofanywa na Marekani na utawala wa Tel Aviv za kuifuta Palestina katika jiografia ya kisiasa ya eneo na dunia.

Amesisitiza kuwa, “Palestina ni ufunguo wa utulivu na usalama wa kikanda. Kwa hivyo, mpango wowote unaopuuza haki za taifa la Palestina ni chanzo cha kukosekana kwa utulivu na kuvuruga usalama wa kikanda.”

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amesema sera ya ujirani mwema inafuatiliwa na serikali  ilioko  madarakani Iran, na kusema kwamba Tehran inataka kukuza zaidi ushirikiano wa pande kadhaa na wa kieneo.

Bagheri Kani amepongeza kuimarishwa uhusiano wa pande mbili za Tehran na Doha Iran inakaribisha  jitihada za Qatar za kuunga mkono sera ya ujirani mwema.

Kwa upande wake, Khulaifi ameashiria mambo ya kihistoria yanayofanana kati ya Qatar na Iran na kuashiria kuongezeka uhusiano wa pande mbili kati ya nchi hizo mbili za Kiislamu katika nyanja zote.

Mwanadiplomasia huyo wa Qatar alisisitiza kwamba mikutano na mashauriano kati ya wanadiplomasia kutoka nchi hizo mbili yatatoa msingi wa kupanua zaidi uhusiano huo.

Wapalestina wanataka Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kuwa sehemu ya taifa huru la baadaye la Palestina, na mji mkuu wake ni al-Quds Mashariki.

Duru ya mwisho ya mazungumzo kati ya Israel na Palestina ilisambaratika mwaka 2014 kutokana na utawala haramu wa Israel kuendeleza sera za kikoloni za kupora zaidi ardhi za Palestina na kujenga vitongoji harmau vya walowezi wa Kizayuni.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *